Dar es Salaam. Hatua ya Tamisemi kuongeza simu mbili kusikiliza rufaa za walioenguliwa kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa imewaibua wadau wa uchaguzi huo wakitaka waliokatwa warejeshwe wote pasipo masharti.
Miongoni mwa wadau hao ni vyama vya siasa, ambavyo vimeitaka Serikali iwawajibishe wasimamizi wa uchaguzi na wasaidizi wao waliowaengua maelfu ya wagombea bila kufuata sheria na kanuni za uchaguzi.
Kwa upande wao, wachambuzi wa masuala ya siasa wamesema taarifa ya Mohamed Mchengerwa, waziri wa nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa iliyoongeza muda na kusahihisha baadhi ya makosa, inaonyesha Tanzania haina mifumo imara ya kusimamia uchaguzi.
“Kama watu wameenguliwa kikanuni, inakuwaje mtu anasimama anasema kanuni zitenguliwe? Tena aliyetoa kauli hiyo ni CCM ambao ni washindani katika uchaguzi, maana yake ni kwamba anayeshindana, anamwambia refa amua hivi,” amesema mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Dk Revocatus Kabobe.
Hoja ya Dk Kabobe inatokana na kauli ya Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi Novemba 12, 2024, ya kuiomba Wizara ya Tamisemi “kupuuza makosa madogo-madogo kwa wagombea na kuwarejesha ili kuleta ushindani na kukuza demokrasia.”
Dk Nchimbi alisema hayo alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, akisema demokrasia ya Tanzania bado ni changa hivyo wagombea walioenguliwa kwa kasoro ndogo-ndogo wapewe nafasi waendelee kujifunza.
Alitoa kauli hiyo wakati baadhi ya vyama vya upinzani vitoa malalamiko ya kuenguliwa kwa maelfu ya wagombea wao.
Kwa mfano, ACT-Wazalendo inadai wagombea wake 51,423 wameenguliwa nchi nzima na CUF kuwa 48,000 kati ya 56,816 waliowasimamisha nchi nzima wameenguliwa.
Chadema inadai takribani nusu ya wagombea wake wameenguliwa japokuwa haijatoa idadi kamili.
Saa chache baada ya kauli ya Dk Nchimbi, Waziri Mchengerwa alitoa taarifa, akiongeza muda wa kamati za rufani za wilaya kupokea, kusikiliza na kutoa uamuzi wa rufaa umeongezwa kwa siku mbili. Muda wa mwisho ulikuwa Novemba 13 na sasa utafikia tamati Novemba 15, 2024 saa 12.00 jioni.
“Ninazielekeza kamati za rufani za wilaya kuitisha fomu za wagombea wote walioenguliwa/hawakuteuliwa ili kufanya mapitio na kujiridhisha na sababu zilizopelekea wagombea hao kutoteuliwa, ili haki iweze kutendeka kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi,” amesema.
Amewaelekeza wasimamizi wa uchaguzi katika halmashauri zote kuwarejesha wagombea wa vyama vyote ambao walienguliwa kwa sababu ya kutodhaminiwa na vyama vyao katika ngazi ya kijiji/mtaa na kuwa vyama hivyo viliwasilisha barua za kuainisha ngazi ya chini ya udhamini kuwa ni kata.
Dk Kabobe akizungumzia kauli za Dk Nchimbi na Mchengerwa, amesema “uchaguzi hauko huru kwa kuwa hakuna sheria mahususi ya kuusimamia kama ilivyoelekeza Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.”
“Kama wagombea walienguliwa kikanuni, hakuna sababu ya kuwarejesha kwani kanuni zipo, lakini kama tunasema tuwarejeshe, ni dhahiri kwamba hatuna mifumo imara ya kusimamia uchaguzi na ndiyo kimekuwa kilio cha muda mrefu tangu mwaka 1992 wakati wa kurejesha mfumo wa vyama vingi,” amesema.
Kuhusu agizo kwa kamati za rufaa kuitisha upya fomu za walioenguliwa, amesema: “Zile kamati zinapaswa kujitegemea na kujisimamia, hazipaswi kuamrishwa au kuelekezwa na waziri kwamba pitieni upya rufaa, hiyo inatoa tafsiri kwamba chaguzi zetu zinaendeshwa na watu wenye mamlaka na si mifumo.
“Tamisemi iko chini ya Rais, Rais mwenyewe na chama chake wana masilahi kwenye uchaguzi, wale wanaosema kwamba wanaosimamia uchaguzi wana upande, utawapingaje?” amehoji.
“Jana Dk Nchimbi alisema kwamba amezungumza na mwenyekiti wa chama na si Rais. Je, mwenyekiti wa ACT-Wazalendo au NCCR-Mageuzi au Chaumma akitoa maelekezo kwenye uchaguzi yangefuatwa?” amehoji.
Kwa upande wake, Profesa wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Bakari Mohamed amesema hakuna mfumo wa kusimamia kanuni za uchaguzi wala kuwawajibisha watendaji wanaosimamia uchaguzi.
“Wasimamizi wa uchaguzi ndio wanajua sababu za kuwaengua wagombea, lakini ukifuatilia asilimia zaidi ya 90 ya sababu hizo hazina mashiko.
“Ili uchaguzi uwe huru na wa haki ni lazima tuwe na mabadiliko makubwa ya Katiba na mifumo ya kusimamia uchaguzi. Pia, kunatakiwa kuwa na mabadiliko kwa vyombo vya ulinzi na usalama, kwa sababu navyo vinahusika katika uchaguzi,” amesema.
Baadhi ya vyama vya siasa vimetoa matamko vikitaka wagombea wake walioenguliwa warejeshwe wote pasipo masharti.
Taarifa iliyotolewa leo Novemba 13 na Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu imesema “hatua ya kuwarejesha wagombea wetu wote walioenguliwa bila sababu ni hatua muhimu, tunaitaka Tamisemi isimamie maelekezo yake kikamilifu kwa sababu tumeshuhudia wasimamizi wa uchaguzi wakidharau maelekezo ya kikanuni,” amesema.
Pia ameitaka Serikali kuhakikisha haki inatendeka katika hatua muhimu zilizobaki za uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji, ikiwemo kampeni, uapishaji mawakala, upigaji kura hadi kutangazwa washindi.
“Pamoja na nia njema ya kuhakikisha demokrasia inastawi kufuatia maelekezo yaliyotolewa, haturidhiki na mtindo huu wa kufanya kazi kwenye mambo ya msingi kwa kusubiri utashi wa maelekezo. Uchaguzi ni mchakato wa kisheria na kikanuni na siyo hisani.
“Tanzania lazima itoke sasa kwenye demokrasia ya kupewa na badala yake tujenge demokrasia iliyosimikwa kwenye misingi ya kikatiba, sheria na kanuni, demokrasia ya maelekezo ndiyo imetufikisha hapa tulipo na lazima tutoke hapa, miaka zaidi ya 30 tangu mfumo wa vyama vingi kuanza,” amesema.
Chadema mbali na kueleza wagombea wake warejeshwe, imetaka pia hatua zichukuliwe kwa wote waliobainika kuwaengua wagombea kinyume cha kanuni.
Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema ameeleza hayo leo Novemba 13, katika taarifa kwa vyombo vya habari.
Amewaagiza wagombea wasiopata fursa ya kuwasilisha rufaa zao kufanya hivyo baada ya muda kuongezwa na Tamisemi.
“Tunatoa wito kwa Tamisemi kuchukua hatua kwa wale watakaobainika kuengua wagombea kinyume cha kanuni ili iwe fundisho na kurejesha amani kwamba wakati wa uchaguzi wasimamizi hao hawatawangaza ambao hawajashinda,” amesema.
Katika hatua nyingine, Mrema ametaka Tamisemi kueleza vigezo vilivyotumika kuchagua vituo vya kupiga kura, akidai vipo vingi na vingine havijulikani kwenye mitaa.
Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Bara), Magdalena Sakaya ameonyesha kutokuwa na imani na kauli ya Waziri Mchengerwa, akisema haitaleta matokeo chanya katika mchakato huo kwa sababu hakufanya utafiti wa kutosha kuhusu mwenendo huo.
“Angetakiwa afanye utafiti wa kutosha wa kujua wagombea wengi wameenguliwa kwa sababu zipi ili kuandika barua yenye tija zaidi, lakini yeye ameelekeza wale waliojaza mihuri yake kata ndio warejeshwe sasa sababu zipo nyingi sana ambazo hazina kichwa wala miguu,” amesema.
Pamoja na malalamiko ya wapinzani, mwanasheria John Seka amewashauri kuzidi kupambana kwenye rufaa.
“Hivi sasa wanaenda ngazi ya rufaa katika kamati za rufaa, wapambane mpaka hatua ya mwisho. Inawezekana wengi wao watarudi katika ngazi hizo. Mchakato wa kuenguana si mchakato rahisi, kwa hiyo bado wana nafasi kubwa ya kuruhusiwa,” amesema.