Dar es Salaam. Tanzania imewahakikishia mabalozi wa mataifa ya kigeni nchini kuhusu uthabiti wa hali ya kisiasa, ufanisi wa mfumo wake wa kodi na uwekezaji, ikisema Serikali inafanya juhudi kubwa kuboresha hali hiyo.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mahmoud Thabit Kombo, amesema hayo leo Novemba 13, 2024 katika kipindi ambacho Taifa linaendelea na maandalizi ya uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 27, 2024, ambao umeibua malalamiko kutoka vyama vya upinzani kuhusu wagombea kuenguliwa.
Kuhusu ushughulikiaji wa mfumo wa kodi, yamekuwapo malalamiko kutoka kwa mabalozi wa mataifa ya Uingereza, Marekani, Uholanzi, Ireland, Ufaransa, Ubelgiji, Canada, Korea, Sweden na Ujerumani ambao katika barua Juni 26, 2024 kwenda Wizara ya Mambo ya Nje, walilalamikia wawekezaji wa kigeni kutoka nchi zao kukaguliwa mara kwa mara na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Rais Samia Suluhu Hassan ameshaunda Tume ya Rais ya Kutathmini na Kushauri kuhusu Mfumo wa Kodi nchini.
Balozi Kombo amesema hayo wakati wa kikao na mabalozi leo Novemba 13, akieleza Tume inajua malalamiko yanayohusiana na mfumo wa kodi, kwa biashara na uwekezaji wa kigeni na wa ndani.
“Mnajua kuwa tume sasa imeundwa kikamilifu na inatekeleza jukumu la kupitia kwa kina sera za kodi na taratibu za kiutawala, kwa kushirikiana na wadau muhimu ili kutoa mapendekezo ya marekebisho ya mfumo wa kodi,” amesema.
Amewashauri mabalozi kuwa na subira, akisisitiza umuhimu wa kushirikiana na mamlaka husika katika masuala hayo.
“Nawaomba kuwa na subira na kushirikiana kwa karibu na mamlaka zote zinazohusika ambazo zimepokea maoni yenu na yote yatakayofuata yaliyothibitishwa na ushahidi,” amesema.
Balozi Kombo amesisitiza juhudi za pamoja kati ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na TRA katika kuandaa mkutano wenye mafanikio na wawekezaji wa kigeni.
“Nadhani mkutano uliofanyika Oktoba, Dar es Salaam ulikuwa fursa muhimu ya majadiliano yenye maana. Ulitoa jukwaa la kujadili masuala yenu na kutafuta suluhisho za pamoja. Huu ni uthibitisho wazi wa juhudi za pamoja za taasisi za Serikali yetu kutatua changamoto zinazowakabili wawekezaji wa ndani na wa kigeni,” amesema.
Amewashauri mabalozi wa kuwasiliana moja kwa moja na mamlaka badala ya kutumia mitandao ya kijamii au majukwaa ya umma kupeleka malalamiko yao.
Amewahakikishia mabalozi kuwa matokeo ya mkutano huo yatakuwa na mchango mkubwa kwa kazi ya tume.
“Nataka kuwahakikishia kuwa ripoti kutoka kwenye mkutano itakuwa mchango muhimu kwa tume. Rais amejipanga kikamilifu na mchakato huu tangu siku ya kwanza madarakani na ameendelea kutoa msaada kwa sekta binafsi na biashara,” amesema.
Kuhusu hali ya kisiasa nchini, Balozi Kombo amesema Tanzania daima imekuwa Taifa lenye utulivu na itaendelea kutilia mkazo uthabiti wa kisiasa wakati wa mchakato wa uchaguzi ujao.
“Tanzania imekuwa na itaendelea kuwa Taifa lenye utulivu, linalozingatia misingi ya utawala bora, haki za kiraia, na michakato ya kidemokrasia,” amesema.
Amezungumzia falsafa ya Rais Samia ya 4R (maridhiano, mabadiliko, ustahimilivu na kujenga upya) akisema ni kiini cha ajenda ya kidemokrasia na utawala bora ya Taifa.
“Falsafa hii ni muhimu katika mbinu yetu ya utawala bora na demokrasia,” amesema.
Kuhusu uchaguzi wa serikali za mitaa wa Novemba 27 na uchaguzi mkuu wa mwakani, amewahakikishia mabalozi kuwa mchakato wa uchaguzi utakuwa huru, haki, wazi, ukijumuisha vyama vingi na hautaharibu utulivu wa nchi.
“Uchaguzi huu hautaleta usumbufu katika amani na utulivu wa kijamii, kiuchumi, na kisiasa,” amesema.
Mkutano huo pia umejadili mapitio ya sera za kigeni, masuala ya ushirikiano wa kikanda na Umoja wa Afrika, pia uhusiano wa kimataifa.