Rais mteule wa Marekani, Donald Trump amemteua mmiliki wa mtandao wa kijamii wa X na mwanateknolojia, Elon Musk kuongoza idara ya ufanisi wa serikali.
Taarifa ya uteuzi huo imetolewa na rais huyo mteule jana Novemba 12, 2024 na kupostiwa katika mitandao yake ya kijamii, kisha Musk naye aliiposti kwa mara nyingine katika ukurasa wake.
Mbali na Musk, pia idara hiyo ambayo itaongozwa na aliyewahi kuwa mgombea wa chama cha Republican, Vivek Ramaswamy.
Tovuti ya Guardian imeandika kuwa licha ya jina hilo, idara hiyo haitakuwa wakala wa serikali. Trump alisema katika taarifa yake kwamba Musk na Ramaswamy watafanya kazi kutoka nje ya serikali, kutoa ushauri na mwongozo wa ikulu na watashirikiana na Ofisi ya Usimamizi na Bajeti.
Trump alisema “wawili hao watafungua njia kwa utawala wangu kufuta urasimu wa serikali, kupunguza kanuni za ziada, kupunguza matumizi yasiyo na msingi na kurekebisha mashirika ya umma.”
Donald Trump alishinda uchaguzi wa Marekani hivi karibuni kwa kupata kura 277 za wajumbe wa uchaguzi, akimshinda mpinzani wake Kamala Harris aliyepata kura 224. Kwa upande wa kura za wananchi, Trump alipata jumla ya kura 71,893,989, sawa na asilimia 51.0, huku Harris akipata kura 67,039,247, sawa na asilimia 47.5.