UWT KIBAHA MJI YAWAPA UJASIRI WA KUSHIRIKI UCHAGUZI WANAWAKE KATA YA MKUZA

NA VICTOR MASANGU, KIBAHA

Jumuiya ya umoja wa wanawake wa chama cha mapinduzi (UWT) Wilaya ya Kibaha mji imeamua kufanya ziara maalumu kwa ajili ya kuwahimiza wanachama wao kuhakikisha kwa sasa wanavunja makundi yote na badala yake wanapaswa kuungana kwa pamoja kwa ajili ya kushinda kwa kishindo katika uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27 mwaka huu.

Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Kibaha mjini Elina Mgonja wakati alipofanya ziara yake maalumu yenye lengo la kukutana na baadhi ya wanawake wa kata ya Mkuza kwa ajili ya kujadili mambo mbali mbali ikiwemo suala la kutoa msisitizo wa kuvunja makundi pamoja na kuwapa hamasa wagombea ambao wameteuliwa na chama kuweza kujitosa katika uchaguzi huo bila woga.

Ziara hiyo ambayo imewakutanisha viongozi mbali mbali wa UWT Kata ya mkuza pamoja na baadhi ya wanawake wengine ambao wameteuliwa na chama kwa ajili ya kupeperusha bendera ya CCM katika uchaguzi wa serikali za mitaa na kuwakumbusha wale wote ambao wameshindwa katika kura za maoni wawe mstari wa mbele kwa ajili ya kuweza kuwasapoti kwa kiasi kikubwa wale ambao wameteulina kugombea katika nafasi mbali mbali.

“Mchakato wa kura za maoni umemalizika katika chama na ndio maana mimi kama Mwenyekiti wenu wa UWT nimeambatana na katibu kwa lengo la kufanya ziara hii na kutoa hamasa ya wagombea wote wanawake ambao wameweza kuteuliwa na chama kutorudi nyuma na kwamba wawe mstari wa mbele wa kuweza kujitokeza katika nafasi zao ambao wanaziwania katika uchaguzi wa serikali za mitaa ikiwemo pamoja na kuvunja makundi ambayo yalikuwepo hapo nyuma,”alisema Mwenyekiti Mgonja.

Mwenyekiti huyo aliongeza kwamba lengo lao kubwa kama UWT ni kuendelea kupita katika maeneo mbali mbali kwa ajili ya kuwahimiza wanawake wote ambao wameteuliwa na chama kuhakikisha wanaweka misingi imara katika kukilindana kukiteteaa chama hivyo wanapaswa kujitokeza kwa wingi bila woga wowote katika zoezi zima la uchaguzi wa serikali za mitaa ili kuweza kuchukua mitaa yote na kushinda kwa kishindo.

Katika hatua nyingine Mgonja aliwahimiza wanawake wote wa UWT katika kipindi hiki cha kuelekea katika uchagzi wa serikali za mitaa kuwa makini sana na kujitahidi kuepukana na propaganda mbali mbali ambazo zinatolewa na vyama vingine vya upinzani na kwamba wazipuuze na waweke misingi na kutokisaliti chama chao.

Kwa upande wake Katibu wa (UWT) Wilaya ya Kibaha mjini Cecilia Ndalu ambaye aliambatana na Mwenyekiti katika ziara hiyo amesema kwamba wanawake ni jeshi kubwa na lengo la chama ni kuhakikisha kwamba inashinda kwa kishindo katika mitaa yote katika uchaguzi huo wa serikali za mitaa.





Related Posts