Wagombea 13 akiwamo mwanahabari wajitosa nafasi ya ukatibu Tucta

Dar es Salaam. Jumla ya wagombea 13 akiwamo mwanahabari, Ebeneza Mende wamejitosa katika kinyang’anyiro cha uchaguzi wa naibu katibu mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), unaotarajiwa kufanyika kesho Alhamisi, Novemba 14, 2024.

Mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi huo, Willy Kibona amesema wagombea hao 13 waliojitokeza kugombea nafasi hiyo wanatoka vyama vya wafanyakazi na kwamba mchakato wa uchaguzi huo unakwenda vizuri.

Amesema uchaguzi huo utafanyikia jijini Dodoma kwa lengo la kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Kornel Magembe aliyeteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Geita, kabla ya kuhamishiwa mkoani Tabora.

Akizungumzia ushindani katika nafasi hiyo, Mende amesema ni wa kawaida na kwamba anayo matumaini ya kushinda nafasi hiyo.

Idadi hiyo ya wagombea imeongezeka baada ya mgombea mmoja aliyekuwa ameenguliwa, Mambo Mkufu ambaye ni mfanyakazi wa Kampuni Tanzu ya Shirika la Umeme (Tanesco) ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji Umeme (ETDCO), kushinda rufaa na kurejeshwa katika kinyang’anyiro hicho.

Alienguliwa na Kamati ya Uchaguzi Tucta katika kikao chake cha Juni 27, 2024 kwa sababu ya kutokuwa na sifa kwa madai hakudhaminiwa na chama chake, Chama cha Wafanyakazi wa Viwanda, Biashara na Taasisi za Fedha na Huduma (Tuico).

Pia, amedaiwa hakuwa na uzoefu wa uongozi ndani ya Tucta wala katika vyama vya wafanyakazi.

Hata hivyo, alikata rufaa katika Kamati ya Utendaji Tucta akidai amewahi kuwa mwenyekiti wa tawi la Tanesco ETDCO miaka saba na mjumbe wa Kamati ya Utendaji mkoa wa Kinondoni Tanesco ETDCO na mjumbe wa Baraza la Wafanyakazi Tanesco ETDCO mpaka sasa.

Pia,alibainisha amedhaminiwa na Tuico na Machi 12, 2024, Tuico ilimwandikia barua iliyosainiwa na Issa Sadallah kwa niaba ya Katibu Mkuu kumjulisha tarehe ya uchaguzi wa nafasi hiyo ambao awali ulikuwa umepangwa kufanyika Machi 22, 2024 mjini Morogoro.

Jana Novemba 12, 2024, Kamati ya Utendaji Tucta katika barua iliyosainiwa na Katibu Mkuu, Hery Mkunda ilimjulisha ameshinda rufaa yake na kwamba amerejeshwa katika kinyang’anyiro hicho, huku ikimtaka ahudhurie uchaguzi huo.

Kuhusu kampeni, Kiboana amesema kwa taratibu zao na kanuni za uchaguzi kwa mujibu wa Katiba ya Tucta, kila mgombea hupewa nafasi ya kujieleza kwa wapigakura siku ya uchaguzi na kueleza sera zake, lakini akasema mgombe hazuiwi kubandika mabango kujitambulisha kwa wapigakura.

“Lakini kampeni huwa ni siku ya kupiga kura, mgombea anasimama na kutoa sera zake na kuomba kura kisha ataulizwa maswali,” amesema Kibona.

“Kwa hiyo kuna haki ya mgombea na haki ya mpiga kura. Baada ya kupiga kura mgombea pia ana haki ya kuteua mwakilishi wake wa kuhesabu kura zake mbele ya kamati ya usimamizi. Kwa ujumla ni haki na wazi.”

Related Posts