Dar es Salaam. Wakulima wa Tumbaku 2,226 kutoka Vyama vya Msingi 22 (AMCOS) mkoani Tabora waliokuwa na mikopo ya Benki ya NMB wamelipwa fidia zao na Kampuni ya Bima ya UAP Sh1.117 bilioni.
Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi hundi, Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amesema NMB na UAP wameonyesha mfano wa kuigwa kwa kukubali kuchukua hatari na kutoa bima za kilimo, sekta aliyoitaja kuwa ngumu zaidi kukopesheka kutokana na wingi wa vihatarishi vinavyoizunguka sekta na wadau wake, hasa wakulima.
Waziri Bashe ametoa pongezi hizo wakati akipokea hundi ya mfano kutoka kwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna, kisha naye kuikabidhi kwa Mwakilishi wa Wakulima na Mwenyekiti wa AMCOS ya USAGUZI, Ally Mrisho, mbele ya Dk Baghayo Saqware, ambaye ni Kamishna wa Mamlaka ya Bima Tanzania (TIRA).
“Kuthibitisha dhamira ya dhati ya NMB katika kukuza sekta ya kilimo, ilitoa mikopo yenye thamani ya Dola milioni 60, takribani Sh150 bilioni. Jumla ya AMCOS 256 zilinufaika na mikopo hiyo, lakini athari zikawafikia wakulima kutoka AMCOS 22, wanaolipwa fidia hii kutoka NMB na UAP,” amesema Bashe.
Ameongeza kuwa, “NMB wamekuwa vinara wa utoaji wa fidia za bima za kilimo na kila mmoja hapa anafahamu kwamba hakuna sekta ngumu kukopesheka kama kilimo, kutokana na vihatarishi vya sekta hiyo, lakini NMB na UAP wamesimama imara kuhakikisha wakulima wanaelewa umuhimu wa bima hizi.”
Amesema Serikali imejipanga katika kufanikisha skimu thabiti ya kilimo, bila hivyo, hakuna mkulima anayeweza kukopesheka, hivyo akaielekeza Tira iharakishe mchakato huo, kwani kila zao lina tabia zake na vihatarishi vyake lakini Serikali inataka kuhakikisha inajenga mfumo wa bima kwa kila zao kulingana na vihatarishi vyake.
Bashe amebainisha ya kwamba tumbaku imekuwa zao muhimu kwa uchumi wa Taifa na kuwa miaka mitatu nyuma Tanzania haikuwa mzalishaji mkubwa, lakini kutokana na mchango wa taasisi za fedha zikiongozwa na NMB, sasa Tanzania ni ya pili kwa uzalishaji wa tumbaku Afrika.
Ameongeza ya kwamba, licha ya athari zilizolipiwa fidia hiyo ya Sh1.117 bilioni, mapato ya jumla ya zao la tumbaku kwa msimu wa 2023/24 ulikuwa ni Sh724 bilioni kutoka Sh717 bilioni za msimu wa 2022/2023 na kwamba msimu huu wa 2024/2025, matarajio ya pato la jumla kwa wakulima linatarajiwa kuwa Sh1.7 trilioni.
Akizungumza katika hafla hiyo, Zaipuna amesema licha ya kukabidhi hundi ya Sh1.117 bilioni ikiwa ni fidia kwa wakulima wa tumbaku na AMCOS mkoani Tabora waliokopa katika benki hiyo, NMB imetenga Sh291.6 bilioni kwa ajili mikopo ya kilimo hicho msimu huu.
Amesema wakulima hao walikatia bima mikopo yao kwa Kampuni ya UAP, na hiyo ni mara ya pili kwa NMB na UAP kutoa fidia ya bima kwa wakulima wa Tumbaku wa Tabora; na mwaka jana walikabidhi fidia ya Sh374 milioni kwa wakulima 400 kwa sababu hizo hizo za hali ya hewa kuathiri kilimo chao.
“Wakulima tunaowafidia leo ni mmoja mmoja na ambao kupitia AMCOS zao, walichukua mikopo ya kilimo cha tumbaku NMB, ambayo ilikuwa na bima kutoka Kampuni ya UAP na hili linakuja baada ya kukamilisha upembuzi na tathimini thabiti na washirika wetu hao,” amesema Zaipuna.
“Wakulima hawa walikumbana na athari za kuharibiwa mashamba na mazao yao katika kipindi cha mvua kubwa pamoja na mvua za mawe, baada ya tathimini kufanywa na wataalamu, ripoti ilitoka na sasa Kampuni ya Bima ya UAP kupitia NMB, tupo tayari kukukabidhi hundi ya fidia hiyo kwa niaba ya waathirika.”
Zaipuna ameishukuru UAP kwa kuhakikisha zoezi hilo linakamilika kwa wakati na wakulima wanapata stahiki zao na kwamba NMB ndio kimbilio sahihi litakalowasaidia waathirika katika kufuatilia fidia zao za bima, kuzipata ndani ya muda muafaka na kuwawezesha kuendelea na shughuli zao.
“NMB ni sehemu sahihi ya kuchukua mikopo ya kilimo, mnyororo unaojumuisha kilimo chenyewe, uvuvi na ufugaji, kwani tuna riba nafuu ya asilimia tisa tu kwa mwaka na uhakika wa fidia yanapotokea maafa kama haya. Tunaishukuru Wizara ya Kilimo kwa kuendelea kushirikiana vyema na NMB katika sekta ya kilimo,” amesema.