Moshi. Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro linamshikilia mfanyabiashara Deogratius Mbuya (40), mkazi wa Kijiji cha Leghomulo, Kata ya Kilema Kusini, Wilaya ya Moshi, mkoani humo akituhumiwa kumuua baba mkwe wake, Tibrus Mnenei (72) kwa kumshambulia kwa panga sehemu mbalimbali za mwili wake.
Mtuhumiwa huyo anadaiwa kutenda kosa hilo wakati alipomfuata mke wake nyumbani kwa wazazi wake alikokwenda wiki iliyopita baada ya kutofautiana.
Inadaiwa kuwa baada ya wawili hao kutofautiana, mkewe alirudi kwa wazazi wake kijijini hapo, ndipo Novemba 13, 2024, mwanaume huyo alipomfuata na kwamba alipofika nyumbani hapo aliulizwa na wazazi wa binti kwanini amefika nyumbani hapo bila kufuata utaratibu.
Baada ya baba mkwe wake huyo kumuuliza hivyo, mwanaume huyo alimwambia anakwenda halafu atarudi tena, na muda mfupi baadaye alirudi akiwa na panga mkononi, ndipo alipoanza kuwashambulia wazazi wa mkewe na baba mkwe alifariki huku akimjeruhi mama mkwe wake kwa kumkata mkono wa kushoto.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amethibitisha kutokea kwa tukio hilo jana Novemba 13, 2024 wakati wakisuluhisha mgogoro wa ndoa.
Kamanda Maigwa amesema chanzo cha tukio hilo ni ugomvi uliotokea wakiwa kwenye kikao cha usuluhishi cha familia kutokana na mgogoro wa ndoa kati ya mtuhumiwa na mke wake, akimtuhumu mke wake kuwa anatoka nje ya ndoa baada ya mtuhumiwa kufanyiwa upasuaji kutokana na matatizo ya kiafya.
“Baada ya usuluhishi kushindikana, mtuhumiwa alianza kumjeruhi mama mkwe wake mkono wa kushoto na baba mkwe alipojaribu kumwokoa, ndipo mtuhumiwa alianza kumkata baba mkwe na kitu chenye ncha kali maeneo ya kichwani, shingoni na mkononi na kumsababishia kuvuja damu nyingi na kusababisha kifo chake.
“Mtuhumiwa baada ya kutenda tukio hilo, alitoroka na msako mkali uliendelea kwa kushirikiana na wananchi, hivyo tumefanikiwa kumkamata akiwa amejificha kwenye jengo ambalo hawaishi watu, akiwa hawezi kuongea na amelazwa KCMC kwa matibabu,” amesema Kamanda Maigwa.
Akielezea tukio hilo, Mwenyekiti mstaafu wa kijiji hicho, James Kyara amesema tukio hilo lilitokea Novemba 13, 2024 baada ya mwanaume huyo kumfuata mkewe nyumbani kwa wazazi wake na kutaka kumchukua na kuondoka naye.
“Huyu kijana alikuwa na mgogoro na mke wake, baadaye walishindwana na mwanamke akaamua kurudi nyumbani kwa wazazi wake. Juzi, walitaka kwenda kuzungumza na kusuluhisha mgogoro wa hawa wawili lakini wazazi walikataa kwa kuwa kijana hakufuata utaratibu,” ameeleza Kyara.
Amesema baada ya wazazi kukataa kijana huyo kurudi nyumbani na mkewe pamoja na mtoto wao mmoja, kijana huyo aliondoka na aliporudi tena nyumbani kwa wazazi hao, alianza kuwashambulia kwa panga.
“Wazazi wa huyu binti walimkatalia kijana kurudi nyumbani na mke wake baada ya kijana kushindwa kufuata utaratibu, baada ya wazazi kukataa alirudi nyumbani kwake kwenda kuchukua panga, aliporudi alimkata mama mkwe mkono upande wa kulia, mume wake alipoona mke wake anauliwa alikwenda kuamua ndipo kijana alipoanza kumshambulia baba mkwe wake kwa kumkata panga sehemu za mkononi, shingoni na kifuani hadi kufa,” amesema Kyara.