AICC Arusha, wapangaji hapatoshi kisa notisi kuachia nyumba

Arusha. Kituo cha Mikutano ya Kimataifa Arusha (AICC) imeingia kwenye mgogoro mkubwa na wapangaji wake zaidi ya 450 baada ya kuwapatia notisi ya kutakiwa kuhama katika nyumba zao ndani ya siku 60 hadi 90.

Wapangaji hao walioishi ndani ya nyumba hizo zilizoko eneo la Kijenge jijini Arusha kwa zaidi ya miaka 40, wamedai kuwa hawatahama katika nyumba hizo kwa sababu ya muda waliopatiwa ni mdogo huku wakidai AICC haijawatendea hai.

Pia, wanadai hawakushirikishwa katika hilo, wakiamini kuwa suala la kuhama ni la majadiliano baina ya pande zote mbili.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi Novemba 14, 2024 eneo zilipo nyumba hizo, mpangaji aliyejitambulisha kwa jina la Deepak Teja amesema kapatiwa notisi ya kuhama ndani ya siku 60, kitendo alichosem ni kigumu kwake.

Amesema kama AICC ingewashirikisha mapema, wangeweza kujadaliana nini cha kufanya na kufikia makubaliano.

“Mimi nimeishi hapa zaidi ya miaka 35 na wapo wengine kwa miaka 40, tumekuwa tukilipa kodi na kuchangia mapato ya serikali bila shida yoyote. Sasa inakuwaje leo hii tunatakiwa kuhama kana kwamba sisi ni wakimbizi, eti kwa sababu tu kuna mradi wanataka kuanzisha? Kwa nini hawakutushirikisha ili tufikie makubaliano ya amani? Hatuondoki hapa mpaka watakapokuja kutupa maelezo ya sababu ya uamuzi huu wa ghafla,” amesema.

Hata hivyo, Mwananchi imezungumza leo na Assah Mwambene ambaye ni Ofisa Uhusiano wa AICC na amethibitisha kuwa taarifa hizo ni za kweli.

Mwambene amesema AICC imeshawakabidhi  barua hizo za notisi  wapangaji wote ikiwataka kuhama ndani ya siku 60  mpaka 90 kupisha eneo hilo kwa ajili ya uwekezaji mpya.

“Hakuna taratibu wala sheria zilizovunjwa kwenye mpango huu. Wapangaji wanatakiwa kuhama ili kupisha mradi huo. Kwa wanaosema hawako tayari kuhama, hatuwezi kusema lolote kwa sasa, ila tutasubiri muda waliopatiwa ukifika taasisi itachukua hatua,” amesema Mwambene.

Akizungumzia sakata hilo, mpangaji Subira Mawenya amesema taarifa hizo zimetolewa kwa ghafla sana na hawawezi kuhama bila mpangilio mzuri.

Hivyo ameiomba AICC kuwapa angalau miezi sita ya kujipanga, akidai muda waliopatiwa unaangukia kwenye msimu wa sikukuu za mwisho wa mwaka na wanahitaji muda zaidi kupata nyumba mbadala kwa familia zao.

“Mimi nina familia kubwa hapa. Ukiniambia nihame kwa siku 60 au 90, unamaanisha kwamba ifikapo Januari niwe nimeondoka. Hebu niambie niende wapi? Tunaomba tuongezewe muda wa angalau miezi sita ili tuweze kuanza mchakato wa kutafuta mahali pengine pa kuhamia,” amesema mpangaji huyo.

Barua ya AICC kwenda kwa wapangaji hao ambayo Mwananchi ina nakala yake, imeeleza  kuwa mkataba wa kukodisha nyumba hizo zilizoko Kijenge umesitishwa ili kupisha utekelezaji wa miradi ya kimkakati katika eneo hilo.

Kwa mujibu wa kipengele cha 4 (vii) cha mkataba wa kukodisha, “Endapo mwenye nyumba atahitaji kurejesha nyumba kwa matumizi yake binafsi, notisi ya siku tisini (90) itatolewa kwa mpangaji kwa anwani iliyooneshwa hapo juu au kwenye mali husika, na baada ya muda huo kuisha, mpangaji atatakiwa kukabidhi nyumba kwa mwenye nyumba,” imeeleza sehemu ya barua hiyo na kuongeza;

“AICC inakupa notisi ya siku tisini (90) ya kusitisha mkataba wako wa kukodisha kuanzia tarehe ya kupokea barua hii ili kupisha utekelezaji wa miradi ya kimkakati katika eneo hili. Tafadhali hakikisha kuwa umeondosha mali zako zote na kukabidhi nyumba hiyo ifikapo tarehe husika.”

Related Posts