AKILI ZA KIJIWENI: Mabeki wa kati ndio silaha yetu Tanzania

KUNA eneo ambalo tumefanikiwa sana kama taifa kuzalisha wachezaji wa kiwango cha juu ambao wamekuwa na manufaa kwa klabu pamoja na timu zetu za taifa.

Eneo hilo ni beki wa kati, kiukweli tuna kila sababu ya kujivunia na katika mjadala wa kijiweni wiki hii tumekumbushana nyakati tofauti zinazodhihirisha namna Tanzania tumebarikiwa kuzalisha mabeki wa kati.

Tujaribu kuanzia miaka ya 2000 hadi sasa kwanza maana ukisema hurudi hadi huko nyuma tutakuwa tunawachanganya vijana  waliozaliwa juzijuzi ambao hawajawaona wazee waliowahi kutamba kwenye soka hapo nyuma.

Katika miaka ya mwanzoni mwa 2000, tulipata mabeki kama Boniface Pawasa, Amri Said, Omary Kapilima, Shaban Ramadhan na John Mwansasu ambao kiukweli walikuwa wanaliumiza kichwa sana benchi la ufundi la timu ya taifa ‘Taifa Stars’ katika uteuzi na upangaji wa kikosi cha timu ya taifa.

Kikaja kizazi cha kina Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Salum Sued ‘Kussi’, Hamis Yusuph, Erasto Nyoni, Dickson Daudi na Aggrey Morris ambacho nacho kilikuwa kinawatesa sana makocha wa Taifa Stars katika maamuzi kuhusu nani awemo na nani asiwemo.

Halafu kikaja kizazi cha kina Juma Nyoso, Kelvin Yondani na kikafutiwa na hawa akina Bakari Mwamnyeto, Dickson Job, Ibrahim Hamad ‘Bacca’, Abdulrazack Hamza, Ibrahim Ame, Abdallah Heri ‘Sebo na Lameck Lawi.

Wahenga walisema hamadi kibindoni na silaha mkononi wakimaanisha kile ambacho kiko karibu yako au unachokimudu ndicho unatakiwa ukitumie kikamilifu ili kiweze kukusaidia.

Kama tuna bahati ya kuzalisha mabeki wazuri wa kati tunatakiwa tuitumie kwa kuhakikisha tunaibua wengi zaidi ili wengine tuwapeleke nje ya nchi wakapate malisho bora zaidi huko ambayo yatakuwa na faida kwetu.

Nchi nyingi hazijapata bahati ambayo imetuangukia sisi hivyo tunatakiwa tuitumie kikamilifu .

Related Posts