Akutwa amefariki nyumbani kwake baada ya kutoka msibani

Arusha. Silasi Ndosi (38) mkazi wa  Shangarai wilayani Arumeru, Mkoa wa Arusha amekutwa amefariki dunia, huku mwili wake ukiwa na majeraha ya mikwaruzo sehemu za kifuani na mgongoni.

Mbali na mikwaruzo pia mwili huo ulikutwa ukitoka damu puani, masikio, na mdomoni.

Akizungumza leo Novemba 14, 2024 kuhusu kutokea kwa tukio hilo,   Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo amesema kuwa mwili wa Ndosi ulibainika alfajiri ya Novemba 12, 2024 huko nyumbani kwake Shangarai iliyoko wilayani Arumeru.

“Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya Mkoa Mount Meru kwa uchunguzi zaidi kujua chanzo cha kifo chake huku upelelezi ukiendelea,” amesema Kamanda Masejo.

Kaka wa marehemu, Elibariki Ndosi amesema kuwa aligundua mdogo wake amefariki alfajiri wa saa 12 asubuhi wakati alipokwenda nyumbani kwake.

“Tulikuwa naye jana hadi saa tano usiku kwenye msiba wa jirani ambapo tulishiriki shughuli zote za msiba kuanzia kuchimba kaburi hadi kumsitiri jirani yetu na akaenda nyumbani kwake kulala akiwa mzima wa afya,” amesema.

Amesema kuwa waliukuta mwili wa marehemu ukiwa na mikwaruzo mithili ya mtu aliyejikuna sana.

“Huyu mdogo wangu hapa anaishi peke yake na alikuja kulala moja kwa moja hakuna shida tuliyosikia, kinachotushangaza sisi ni kumkuta amekufa kifo chenye utata. Tunaomba polisi na madaktari wachunguze kiini,” amesema.

Amesema kuwa marehemu hakuwa na mgogoro na mtu yoyote zaidi ya aliyekuwa mke wake waliyezaa naye watoto wawili na kuachana ambapo wana kesi mahakamani ya kudaiana talaka sambamba na mgawanyo wa mali.

Related Posts