Josep Borrell alitoa pendekezo lake hilo wakati wa mkutano wa mabalozi na kwa mujibu wa wanadiplomasia wanne waliohusika, mkuu huyo wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya anatarajiwa kulirasimisha pendekezo lake wakati wa mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya utakaofanyika mjini Brussels mapema wiki ijayo.
Mkuu huyo wa sera za kigeni ameziandikia nchi wanachama kuziomba zisitishe mazungumzo ya kisiasa kati ya Umoja wa Ulaya na Israel na mmoja kati ya wanadiplomasia amesema ni kutokana na madai kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu na uvunjaji wa sheria za kimataifa katika vita vya Israel dhidi ya kundi la Hamas.
Msemaji wa Tume ya Ulaya Peter Stan, amesema Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell, atawataka mawaziri wazingatie iwapo Israel inakiuka haki za binadamu, inaheshimu au haiheshimu sheria za kimataifa juu ya haki za binadamu kwa mujibu wa vifungu husika kwenye Makubaliano ya Muungano. Atawataka Mawaziri watoe maoni yao kuhusu pendekezo lake la kuyasimamisha mazungumzo ya kisiasa.
Ni jukumu la mawaziri kuamua iwapo watakubali kuendelea na kulijadili pendekezo hilo la Borrell au la, hili litajulika mapema wiki ijayo watakapokutana na mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels
Soma Pia: Borrell: Vita vya Gaza ni “janga”
Umoja wa Ulaya umegawanyika kuhusu Israel na Wapalestina na kuna uwezekano mkubwa kwamba mawaziri hao watapinga pendekezo la kusitisha mazungumzo hayo, ambayo ni sehemu ya Makubaliano ya Jumuiya ya Umoja wa Ulaya ambayo inasimamia uhusiano kati yake na Israel.
Pendekezo la Borrell amelitoa bila ya tahadhari na limepokewa kwa mshangao mkubwa, kulingana na mwanadiplomasia mwingine ambaye amethibitisha kwamba litapingwa na kundi kubwa la nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya.
Tayari Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock, amesema nchi yake haikubaliani na pendekezo la Josep Borrell la kusimamisha mazungumzo ya kisiasa na Israel ili kukabiliana na vita vya Gaza na nchini Lebanon amesema Ujerumani siku zote inapendelea kuweka njia za mazungumzo wazi.
Mataifa mengine yanayotazamiwa kulipinga pendekezo hilo ni pamoja na Italia, Uholanzi, Denmark, Jamhuri ya Czech, Austria, Hungary na Ugiriki.
Vyanzo: AFP/DPA