CCT yashauri makosa madogo yasiwe sababu kuenguliwa wagombea

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) imeshauri masuala madogo madogo ya kiufundi yasitumike kama sababu ya kuwaengua wagombea ili kutoa haki sawa kwa wagombea wote.

Ushauri huo umetolewa leo Novemba 14,2024 na Mwenyekiti wa CCT, Askofu Dk. Fredrick Shoo, wakati akitoa tamko la jumuiya hiyo kuhusu Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27 mwaka huu.

Amesema wamekuwa wakifuatilia kwa makini mchakato mzima wa uchaguzi huo tangu mwanzo wakishiriki kutoa maoni wakati wa uandaaji wa sheria na kanuni za uchaguzi na kufuatilia maandalizi ya uchaguzi huo.

“Kumekuwa na malalamiko mengi kuhusu kuenguliwa kwa majina mengi ya wagombea kwa makosa madogo madogo kama ya kushindwa kuandika majina matatu, anuani au kasoro ndogo zinazoweza kurekebishwa.

“Tunazitaka mamlaka husika kufanya ufuatiliaji wa kina utakaopelekea kupatikana majibu ili kuondoa taharuki na hofu iliyopo kwenye jamii,” amesema Askofu Dk. Shoo.

Mwenyekiti huyo wa CCT pia ameipongeza Serikali kwa kusikiliza sauti za wananchi na kuelekeza marejeo ya rufaa za wagombea walioenguliwa katika nafasi zao.

Ametoa wito kwa wasimamizi wa uchaguzi kutekeleza majukumu yao kwa uwazi, usawa kwa kuzingatia sheria zilizowekwa bila upendeleo wa aina yoyote.

Dk. Shoo amewasihi waumini na wananchi wote kwa ujumla kudumisha amani na utulivu kabla, wakati na baada ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Amesema wananchi wanapaswa kuepuka vishawishi vyovyote vya kiitikadi au namna yoyote inayoweza kuleta machafuko katika Taifa.

“Tunawahamasisha wananchi wote waliojiandikisha kujitokeza kwa wingi na kutimiza haki yao ya kuchagua viongozi wa kijamii wa mtaa, kijiji na kitongoji wenye sifa sio kwa ushabiki wowote ule…wananchi waendelee kudumisha amani na mshikamano wakati wote wa uchaguzi,” amesema.

Jumuiya hiyo imewahimiza waumini wote kumtanguliza Mungu katika kipindi hiki muhimu cha kuelekea katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa ajili ya maendeleo na ustawi wa Taifa la Tanzania.

Related Posts