Dar es Salaam. Shirika la Reli Tanzania (TRC), limesema limepata fedha kwa ajili ya ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kutoka kipande cha Uvinza mkoani Kigoma hadi Musongati nchini Burundi.
Hayo yamesemwa leo Alhamisi Novemba 14, 2024 na Kaimu Mkurugenzi wa TRC, Mateshi Tito wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), kutembelea na kupokea taarifa ya utekelezaji wa mradi wa SGR.
Tito amesema fedha hizo ni kutoka Benki ya Standard Chartered, Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Kampuni ya Bima ya China (SINO Insuarance).
“Wenzetu hawa wametoa mkopo nafuu na ni fedha zitakazowezesha kukamilisha ujenzi huo kama ulivyopangwa,” amesema.
Ujenzi wa reli hiyo utakapokamilika unatarajiwa kuimarisha huduma za uchukuzi kati ya Tanzania, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Kwa mujibu wa Wizara ya Uchukuzi, ujenzi huo umegawanywa katika sehemu mbili ambazo ni Uvinza hadi Malagarasi kwa upande wa Tanzania yenye urefu wa kilomita 156 na Maragasi-Musongati hadi Gitega yenye urefu wa kilomita 126.
Ujenzi wa reli hiyo utakuwa na manufaa kwa Tanzania na Burundi na utaibua fursa nyingi za ajira na biashara, hivyo kukuza uchumi kwa wakazi wa mataifa hayo.
SGR kwa sasa inafanya kazi ya kusafirisha abira kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro na Dar es Salaam hadi Dodoma.
Akizungumzia ushirikiano na sekta binafsi katika mradi wa SGR, amesema wanaendelea vizuri kwa kuwa wawekezaji wengi wa kigeni na wa ndani wamejitokeza wakitaka kuwekeza.
Tito amesema kilichobaki ni kuendelea kukamilishwa kwa kanuni za ubia katika uendeshaji wa reli hiyo baada ya Bunge kupitisha sheria hivi karibuni.
Awali, Mwenyekiti wa Kamati ya PIC, Augustine Vuma, amesema wametembelea kujionea mradi huo ambao uwekezaji wake wameridhishwa nao.
Vuma amesema tangu treni ilipoanza kusafirisha abiria imeshaingiza Sh20 bilioni, akieleza wanatarajia itakapoanza kusafirisha mizigo itaingiza fedha hizo zaidi ya mara tatu.
“Katika usafiri wa reli mapato yatokanayo na abiria huwa ni asilimia ndogo kama 20 hivi, huku asilimia 80 na zaidi, mara nyingi inatokana na usafirishaji wa mizigo.
“TRC imetueleza kwenye taarifa yao wamejipanga kuanzia mwakani Januari au Februari wataanza kusafirisha mizigo kwenye reli hiyo,” amesema akieleza muda huo mabehewa ya mizigo yanatarajiwa kuwa yamefika nchini.
“Maana yake hapa tunategemea mapato yataongezeka zaidi ya mara tatu zaidi ya ambayo yameshapatikana sasa,” amesema.
Amesema kwa muda mrefu sasa watu wameshachoka kutumia malori kusafirisha mizigo ambayo siyo tu yanaharibu barabara, lakini yenyewe huwa yakiharibika barabarani na kubwa zaidi ni gharama katika kusafirisha mzigo ukilinganisha na kusafirisha na SGR.
Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile amesema kamati imeshauri kukamilishwa haraka kwa vipande vingine vilivyobaki vya SGR ili Watanzania wanufaike kwa kubeba abiria na mizigo ili kupata faida kubwa kama nchi.
Amesema wabunge wamepokea mipango ya baadaye, ikiwamo muunganiko wa sekta hiyo na nyingine. Amesema kilomita 2,300 zinajengwa kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza.
Amesema haiishii hapo, pia wanafanya maboresho ya bandari zikiwamo za Dar es Salaam, Mtwara na za kwenye maziwa yote ili kuhakikisha mzigo unakwenda ng’ambo kirahisi.
Kihenzile amesema Serikali imetenga zaidi ya Sh2 trilioni kwa ajili ya kujenga miundombinu ya meli. Kwa kuanzia Ziwa Tanganyika amesema wanajenga chelezo zenye uwezo wa kujenga meli mbili za tani 5,000 kila moja.
“Tunakwenda kujenga meli nyingine mpya ya mizigo ya tani 3,500 katika Ziwa Tanganyika na kama haitoshi Serikari imeidhinisha fedha ya kufanya ukarabati wa meli takribani zote zilizopo katika Ziwa Tanganyika zikiwemo Mv Liyemba, Mwongozo na Sangara,” amesema.
Kwenye Ziwa Victoria ameeleza kuwa, Serikali imetenga fedha ya kuanza ujenzi wa meli kubwa ya takribani tani 3,000 na kukamilisha meli ya Mv Kazi ambayo imeshakamilika kwa asilimia 97 hadi sasa.