Mkutano huo unafanyika wakati Iran ikifahamisha kuwa, itachukua hatua za haraka za kukabiliana dhidi ya azimio lolote la bodi ya magavana ya IAEA linaloingia mpango wake wa nyuklia.
Shirika la habari la Iran IRNA limeripoti kuwa Grossi, aliyewasili mjini Tehran jana jioni, anatarajiwa kujadiliana na maafisa wakuu wanaohusika na mpango wa nyuklia wa Jamhuri hiyo ya Kiislamu.
Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wake wa kijamii wa X, Grossi ameueleza mkutano wake na Waziri wa mambo ya nje wa Iran Abbas Araghchi kama “tukio muhimu.”
Araghchi alikuwa mpatanishi mkuu wa Iran katika mazungumzo yaliyopelekea kuafikiwa kwa mkataba wa nyuklia wa Iran wa mwaka 2015.
Soma pia: Iran yakanusha madai ya kumuua Trump
Kwa upande wake, Waziri huyo wa mambo ya nje wa Iran amefahamisha kuwa mkutano huo uliangazia mambo muhimu na kusisitiza ahadi ya Iran kwa mkataba wa NPT wa kuzuia kuenea kwa silaha za nyuklia duniani.
Katika ujumbe aliouchapisha, Araghchi amesema wamekubaliana kuendelea na mazungumzo kwa ujasiri na nia njema. Ameongeza kuwa Iran haijawahi kuondoka kwenye meza ya mazungumzo kuhusu mpango wake wa nyuklia aliouita kuwa wa amani.
Mwanadiplomasia huyo wa Iran amesema nchi yake ilikuwa tayari kujadiliana kwa kile alichokiita “misingi ya maslahi ya kitaifa” na “haki zisizoweza kuondolewa.”
Hata hivyo Araghchi amefahamisha kuwa Iran haiko tayari “kujadiliana chini ya shinikizo na vitisho.”
Iran itapinga azimio la kuingilia mpango wake wa nyuklia
Grossi pia amekutana na mkuu wa shirika la nishati ya Atomiki la Iran Mohammad Eslami.
Eslami amewaambia wanahabari katika mkutano wa pamoja na Grossi kuwa azimio lolote la kuingilia kati mpango wa nyuklia wa Iran litakabiliwa na upinzani wa haraka. Baadaye, mkuu huyo wa IAEA anatarajiwa kukutana na Rais wa Iran Masoud Pezeshkian.
Soma pia: Mkuu wa IAEA azuru Kinu cha nyuklia cha Kursk nchini Urusi
Ziara ya Grossi ni ya pili mjini Tehran mwaka huu japo ni ya kwanza tangu kuchaguliwa tena kwa Donald Trump.
Wakati wa muhula wake wa kwanza kutoka mwaka 2017 hadi 2021, kiongozi huyo wa Marekani alionekana kuwa kinara wa kushinikiza kupitishwa kwa sera iliyojulikana kama “shinikizo la juu zaidi” dhidi ya Iran ambayo ilirudisha vikwazo vya kiuchumi vya Marekani vilivyokuwa vimeondolewa chini ya mkataba wa kihistoria wa nyuklia wa mwaka 2015.
Mnamo mwaka 2018, Trump aliiondoa Marekani katika mkataba wa nyuklia wa 2015 kati ya Iran na mataifa ya magharibi ulioipa Iran nafuu dhidi ya vikwazo vya kimataifa.
Mwaka uliofuata, Iran ilianza japo polepole kwenda kinyume na makubaliano ya nyuklia ambayo yaliizuia Jamhuri hiyo ya Kiislamu kuimarisha urutubishaji wa madini ya urani hadi kiwango cha juu cha asilimia 3.65.
IAEA inasema Iran imeongeza kwa kiasi kikubwa akiba yake ya madini ya urani yaliyoboreshwa hadi asilimia 60, kiwango ambacho kimezusha wasiwasi wa kimataifa kwani kinakaribia kiwango cha asilimia 90 kinachohitajika kutengeneza silaha za nyuklia.