Moshi. Ndafu siyo neno geni kusikika masikioni mwa Watanzania wengi, hususani watu wa jamii ya kabila la Wachaga na baadhi ya makabila yanayopatikana kanda ya kaskazini.
Kwa tafsiri halisi, ndafu ni mbuzi dume, (beberu) aliyehasiwa na kukuzwa kwa ajili ya kuandaliwa kama chakula cha heshima.
Lakini umewahi kujiuliza neno ‘ndafu’ linatokana na nini hasa? Mwananchi limezungumza na baadhi ya watu wakiwemo machifu ambapo wamelizungumzia kwa mitazamo tofauti tofauti na kila mmoja akieleza namna anavyofahamu neno hilo.
Kwa Wachaga, ndafu ni chakula cha heshima ambacho huandaliwa kwa watu maalumu wa heshima na kwa sababu maalumu na chakula hicho hutoa ishara ya upendo, amani na mshikamano.
Chakula hicho pia kimezoeleka kuandaliwa wakati wa harusi na hata hafla za kuaga maharusi, ikiwa ni heshima ambayo wazazi humpa mtoto wao anayeenda kuanza safari ya maisha mapya ya ndoa, ambayo humaanisha ni matamu kama hiyo ndafu, lakini wakati mwingine ni magumu kama unavyoitafuna nyama hiyo ya mbuzi.
Pamoja na heshima ya chakula hicho, maswali mengi yamekuwa yakiibuka juu ya chimbuko la neno hilo ‘ndafu’ ambalo ndilo jina limezoeleka kutamkwa inapochomwa nyama hiyo ambayo huandaliwa kwa ustadi mkubwa.
Uchagani nyama hiyo ikishaandaliwa, huwekewa majani mabichi mdomoni na kupelekwa kwa mgeni maalumu, ambapo hukabidhiwa. Baadaye naye hupokea kisha hukaribisha watu kwa ajili ya kula.
Baadhi ya watu wanadai kwamba jina la ndafu lilitokana na mmoja wa kiongozi wa Waingereza aliyekuja kutembea mkoani Kilimanjaro na baada kukaribishwa na machifu alipewa nyama hiyo ya mbuzi iliyochomwa na kuandaliwa kwa heshima, ambapo baada ya kula alisema ‘it’s wonderful’ maana yake nyama nzuri.
Kutokana na maneno hayo kutamkwa kwa lugha ya Kiingereza waliokuwa wakimwandalia, walidhani alitamka ‘ndafu’ na kuanzia siku hiyo wakaiita nyama hiyo ndafu.
Hata hivyo, inaelezwa kuwa neno hilo lilikuwa maarufu tangu miaka ya 1950 na kupewa heshima yake katika jamii nyingi za kanda ya kaskazini hususani uchagani.
Godfriend Kileo ambaye ni Chifu wa Wachaga wa Siha, anasema ili mbuzi iwe ndafu ni lazima awe mbuzi dume aliyehasiwa, kulishwa vizuri na kunenepeshwa, na huandaliwa kwa ajili ya mgeni maalumu wa heshima.
“Ndafu ni mbuzi dume aliyehasiwa akanenepshwa, nyama yake hapo zamani alikuwa anapewa mgeni wa heshima anapokuja kwenye shughuli, hivyo ni chakula cha heshima sana kwa mgeni mwenye heshima,”anaeleza chifu Kileo.
Anasema pamoja na kwamba kwenye sherehe kubwa zinazofanywa na Wachagga kama vile harusi , ubarikio kunakuwepo na ndafu hiyo, mgeni rasmi ndiye hupewa kipaumbele cha kukata ndafu hiyo kutokana na umuhimu wake.
Aidha, anasema lengo kuu la uwepo wa ndafu katika matukio muhimu, ni kwamba chakula hicho ni cha heshima kwa ajili ya kumpa mgeni rasmi na mwenye heshima, akisisitiza kuwa sio kila mtu anapewa.
“Kwa kawaida ndafu huandaliwa kama ishara ya upendo na ni chakula cha heshima ambacho huandaliwa kwa ajili ya mgeni maalumu, na hapo zamani ukitaka kwenda kuomba kitu kwa wazee unakwenda na ndafu hata kama umemkosea baba, ulitakiwa kwenda na ndafu na ukienda naye hata kama anataka kutoka atarudi kukaa kukusikiliza,”anasema Kileo.
Kuhusu asili ya nen hilo, Chifu Kileo anasema ni jina ambalo liliibuliwa na wazee wa zamani likimaanisha beberu.
Gabriel Mollel, ambaye ni Leiguanani wa Wilaya ya Hai, anasema kwenye kabila lao la Wamasai, ndafu ambayo wao huita kwa jina la ‘Orijinee’ wamekuwa wakitumia kama ishara ya upendo pale wanapotaka kuomba kitu kwa wazeee wenye umri mkubwa katika jamii zao.
Kwa upande mwingine anasema wanatumia ndafu kwa kumpongeza mwanamke aliyejifungua, ambaye anapendwa na mumewe kama ishara ya upendo na kumshukuru.
“Sisi Wamasai ndafu tunaiita orijinee, kwetu ndafu ni kama ishara ya upendo, kwa mfano kama mke amejifungua na anapendwa na mume wake, au kwa wazee kama una jambo lako unalotaka kuanzisha au kumuomba ushauri, huwezi kwenda bila chochote na hata ukienda kwa mzee na ndafu hata kama ana haraka kiasi gani, hawezi kukuacha lazima akupokeee na akusikilize,”anasema Mollel.
Mzee Joseph na utata wa asili ya ndafu
Akizungumzia historia ya neno ndafu lilivyoanza, mmoja wa wazee wa Wilaya ya Rombo, Athanas Joseph anasema miaka ya 1950 mmoja wa machifu wa Wachaga, alimkaribisha mgeni aliyetoka nchini Uingereza.
Anasema walimwandalia nyama nzuri na alipomaliza kula akashukuru kwa kusema ‘it’s wonderful’ maana yake kwamba nyama ni nzuri na tamu.
“Mangi alipowakaribisha Waingereza nyama safi ya beberu aliyehasiwa, amenona na aliyeokwa kitaalamu, walipomaliza kula wakasema ‘it’s wonderful’ ndio Mangi alipomuuliza yule aliyemwagiza awafanyie sherehe hiyo, wameitaje hiyo? akamwambia kwa Kichaga wameita ‘ndafu’,”
Anasema ndipo neno hilo, liliponza kutumika na kuwa maarufu kwa Wachagga na baadhi ya watu wa makabila mengine ya ukanda mzima wa Kaskazini.