Dar es Salaam. Saratani ya damu ndio ugonjwa uliokatisha maisha ya aliyekuwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango Tanzania, Lawrence Mafuru (52).
Mtaalamu huyo wa fedha na uchumi maarufu chini humo, alifariki dunia Novemba 9, 2024 akiwa anapatiwa matibabu Hospitali ya Apollo nchini India.
Mwili wa Mafuru unaagwa leo Alhamisi, Novemba 14, 2024 katika viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam ambapo waombolezaji mbalimbali wanashiriki wakiongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Akisoma wasifu wa marehemu, Katibu Mkuu Wizara ya Mipango na Uwekezaji, Dk Tausi Kida amesema Mafuru aliyeacha mke na watoto wawili wa kike alianza kuugua Agosti 2024 na kupatiwa matibabu Hospitali ya Taifa Muhimbili kisha kuhamishiwa Apollo nchini India kwa matibabu.
Amesema Mafuru alizaliwa Juni 20, 1972 mkoani Mara na kusoma elimu ya msingi na sekondari nchini kisha kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Hadi mauti yanamkuta, Mafuru alikuwa ni Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango. Mwili wake utazikwa kesho Ijumaa, Novemba 15, 2024 kwenye makaburi ya Kondo yaliyopo Tegeta jijini Dar es Salaam.
Ibada ya kuaga mwili wake imeongozwa na Askofu Mkuu wa Kanisa la Waadventista Wasabato (SDA), Jimbo la Kasikazini mwa Tanzania, Mchungaji Mark Malekana.
Saratani ya damu ni ugonjwa mbaya ambao huathiri watu na familia nyingi kote duniani.
Saratani ya damu, pia inajulikana kama saratani ya hematological. Huathiri uzalishaji na utendaji wa seli za damu na kusababisha ongezeko lisilo la kawaida la idadi ya seli za saratani.
Seli hizi za saratani zinaweza kugawanywa katika aina kuu tatu, leukemia, lymphoma na myeloma.
Leukemia ni saratani ya damu changamano na kali ambayo hutokea wakati mwili huzalisha seli nyeupe za damu zisizo za kawaida ambazo hazijakua kikamilifu na haziwezi kufanya kazi zinazokusudiwa.
Uzalishaji mwingi wa seli hizi ambazo hazijakomaa unaweza kuvuruga utengenezwaji wa chembe nyekundu za damu na chembe chembe za damu, ambazo ni muhimu kwa kubeba oksijeni na kuzuia kutokwa na damu, mtawalia.
Kuna aina tofauti za saratani ya damu, kila moja ina dalili zake. Walakini, dalili za kawaida za saratani ya damu ni pamoja na kuhisi udhaifu, maambukizi ya mara kwa mara au homa, kupoteza uzito, kutokwa jasho jingi usiku, maumivu ya mifupa, kuvimba maeneo ya shingo, kwapa, kinena, au maumivu ya mifupa, kutokwa na damu kwa urahisi maeneo ya puani au fizi, kushindwa kupumua, kizunguzungu na kupoteza hamu ya kula.
Ikimzungumzia marehemu Mafuru, ofisi ya Msajili wa Hazina alipowahi kufanya kazi kama Msajili wa Hazina imesema alikuwa ni kiongozi aliyemfahamu kila mmoja aliyefanya naye kazi.
Wakiongozwa na Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu ambaye awali amesema hakumkuta Mafuru Hazina, hivyo kutoa nafasi kwa wale waliofanya kazi na Mafuru Hazina kumuelezea.
Mwakilishi wa ofisi ya msajili wa hazina alisema kuja kwa Mafuru, Hazina ilikuwa ni nguvu ya kuchanganya utendaji kazi wa sekta binafsi na umma.
Wamesema pamoja na kuwa mgeni kwenye utumishi, siku ya kwanza aliporipoti ofisini alifanya mahojiano na kila mmoja na alitaka kila mmoja awasilishe wasifu.
“Alipouliza kwanini, akasema anataka kumfahamu kila mtu, aliona uwezo ndani ya kila mmoja, alitoa muda na kueleza kuhusu ‘sprit’ yake ya kufanya kazi na akasema walioko tayari kufanya naye kazi wafanye, ambao hawako tayari warudi wizarani,” amesema.
“Hakupenda kufanya kazi kwa mazoea, alikuwa mtu wa kuimarisha taasisi, miongoni mwa mengi aliyoyafanya ni pamoja na kuongeza idadi ya mashirika yanayochangia asilimia 15 na taasisi zinapokea rukuzu kuchangia mfuko mkuu wa Serikali.
Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari zaidi