Dar es Salaam. Wataalamu wa magonjwa ya saratani wamesema ugonjwa wa saratani ya damu ‘Leukemia’ hauna chanzo maalumu, huku wakitaja sababu za kimazingira zinazoweza kuchangia mtu kupata ugonjwa huo.
Saratani ya damu ndio ugonjwa uliokatisha maisha ya aliyekuwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango Tanzania, Lawrence Mafuru (52).
Mtaalamu huyo wa fedha na uchumi maarufu nchini humo, aliyefariki dunia Novemba 9, 2024 akiwa akipatiwa matibabu Hospitali ya Apollo nchini India, anatarajiwa kuzikwa kesho Ijumaa Novemba 15, 2024 kwenye makaburi ya Kondo, Tegeta jijini Dar es Salaam.
Ingawaje wagonjwa wengi hupata leukemia, saratani ya damu huathiri uzalishaji na utendaji wa seli za damu na kusababisha ongezeko lisilo la kawaida la idadi ya seli za saratani zinazoweza kugawanywa katika aina kuu tatu, leukemia, lymphoma na myeloma.
Leukemia ni saratani ya tishu zinazounda damu za mwili, pamoja na uboho na mfumo wa limfu. Leukemia inaonekana kwa watu wazima na watoto na katika wagonjwa hao uboho hutoa seli nyeupe za damu zisizo za kawaida.
Akizungumza na Mwananchi leo Alhamisi, Novemba 14, 2024, Daktari bingwa mbobezi wa magonjwa ya saratani kutoka Hospitali ya Aga Khan, Steven Chuwa amesema hakuna visababishi maalum vya kimaumbile isipokuwa vya kimazingira akisisitiza saratani hiyo si miongoni mwa saratani 10 zinazoongoza nchini.
“Hakuna sababu maalumu, kuna mambo mengi lakini kikubwa zaidi mionzi inayosambaa inasababisha hiyo saratani ya damu. Kwa mfano majanga ya bomu la nyuklia yaliyotokea kule Japan, nyuklia plant kule Ukraine ilivyoharibika ikavuja wale watu wanapata saratani za damu,” amesema Dk Chuwa.
Dk Chuwa amesema kuna uhusiano wa moja kwa moja na watu wanaofanya kazi kwenye viwanda vya rangi, kutokana na baadhi ya malighafi zinazotumika kutengenezea bidhaa hiyo.
“Zaidi ni bahati mbaya inamkuta mtu, hakuna sababu maalumu ya moja kwa moja, zaidi ni mabomu ya nyuklia au mtambo wa kuzalisha umeme wa nyuklia, ikitokea ajali wale watu wakakutana nayo wapo kwenye hatari ya kupata leukemia,” amesema.
Hata hivyo, Dk Chuwa amesisitiza kuhusu kemikali za kutengenezea rangi, akisema huleta athari mpaka mtu awe amefanya kazi kwa muda si jambo la siku moja.
Leukemia ni saratani ya damu changamano na kali ambayo hutokea wakati mwili huzalisha seli nyeupe za damu zisizo za kawaida ambazo hazijakua kikamilifu na haziwezi kufanya kazi zinazokusudiwa.
Uzalishaji mwingi wa seli hizi ambazo hazijakomaa unaweza kuvuruga utengenezwaji wa chembe nyekundu za damu na chembe chembe za damu, ambazo ni muhimu kwa kubeba oksijeni na kuzuia kutokwa na damu, mtawalia.
Kuna aina tofauti za saratani ya damu, kila moja ina dalili zake. Walakini, dalili za kawaida za saratani ya damu ni pamoja na kuhisi udhaifu, maambukizi ya mara kwa mara au homa, kupoteza uzito, kutokwa jasho jingi usiku, maumivu ya mifupa, kuvimba maeneo ya shingo, kwapa, kinena au maumivu ya mifupa, kutokwa na damu kwa urahisi maeneo ya puani au fizi, kushindwa kupumua, kizunguzungu na kupoteza hamu ya kula.
Saratani ya damu imeelezwa kuchangia vifo vya watoto wengi wanaogundulika kuugua ugonjwa huo, ambao hukutwa katika hatua za tatu na nne za ugonjwa hali inayosababisha asilimia 90 yao kutopona.
Wataalamu wamesema asilimia kubwa ya watoto hufariki dunia wakiwa majumbani au katika hospitali za chini, wakitaja dalili za saratani ya damu kwa kundi hilo ni mtoto kupata homa ya mara kwa mara, kukonda, kulia sana, kuishiwa damu mara kwa mara.
Daktari bingwa wa magonjwa ya watoto aliyebobea katika tiba ya saratani na damu kwa watoto, Lulu Chirande amesema kwa wastani inakadiriwa watoto 300,000 kila mwaka duniani wanapata saratani ya damu.
Amesema kwa Tanzania wanaofanikiwa kufika hospitali ni 800 ambao wanachunguzwa na majibu yanatoka kwamba ni saratani ya damu na kwa Hospitali ya Taifa Muhimbili peke yake ni watoto 500 wanagundulika kila mwaka.
“Tatizo ni kubwa kwani wengine wanafariki wakiwa majumbani. Asilimia 90 yao wanafika katika hatua za nne na tatu za ugonjwa hali inayosababisha tiba kuwa ngumu na wengi wanafariki lakini mzazi akiwahi kumbaini mtoto akamleta katika hatua za kwanza za ugonjwa au hatua ya pili wanatibiwa na kupona kabisa.
“Wengi hawafiki wanaishia katika hospitali za chini ambazo hazina wataalamu wa kutosha wanatibu baadaye wanafariki,” amesema Dk Chirande.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Sayansi Muhimbili (Muhas), Profesa Andrea Pembe amesema mpaka sasa bado hakuna takwimu kamili na kwa sasa wataalamu wanajiandaa kufanya utafiti utakaobaini nchi ina watoto wangapi wanaougua ugonjwa wa saratani ya damu.
“Hatuna takwimu kamili saratani ya damu kwa watoto ni tatizo kubwa kwa sasa, lakini hatujajua kama kuna ongezeko la wagonjwa wa saratani au uwezo wetu wa utambuzi umeongezeka kwa ujumla namba yao inaongezeka nchini. Utafiti utatuambia,” amesema Profesa Pembe.