Israel yalaumiwa kwa kutenda uhalifu wa kivita – DW – 14.11.2024

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limesema katika ripoti yake iliyotolewa hii leo Alhamisi kwamba wapalestina katika Ukanda wa Gaza, wakati wote wamelazimika kuyahama makazi yao kutokana na operesheni ya kijeshi ya Israel kwa kiwango ambacho kinatosha kusema kuwa ni uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu.

Soma Pia: Israel yatakiwa kutekeleza hatua za kusitisha mapigano Gaza  

Ripoti hiyo ni ya hivi punde zaidi katika mfululizo wa ripoti zinazochapishwa na makundi ya misaada na mashirika ya kimataifa yanayoonya kuhusu hali mbaya ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza unaozingirwa.

Familia za Wapalestina
Wapalestina katika eneo la Beit Hanoun, wakimbia vita kutoka kwenye eneo hilo la kaskazini mwa Ukanda wa GazaPicha: Hadi Daoud/APAimages/IMAGO

Nadia Hardman, Mtafiti, katika Kitengo cha Haki za Wakimbizi na Wahamiaji, cha Human Rights watch amesema:

“Tumefahamu na tumesikia kuhusu, jinsi Israel inavyowahamisha watu kwa kigezo cha usalama wao. Imetoa, mamia ya maagizo ya kuwataka watu waondoke kwenye maeneo kadhaa. Tulichofanya, sisi HRW, tumezifuatilia amri hizo za kuwahamisha watu na tumeyaangalia maagizo 184 kati ya mengiyaliyotolewa na yameonyesha jinsi ambavyo hayaendani na sheria na pia hayaeleweki. Njia salama zilishambuliwa, maeneo salama yalishambuliwa na hakuna mahali salama pa kuwapeleka watu. Ni muhimu kuyapinga madai ya Israeli kwamba inatii sheria za vita. ”

Katika ripoti hiyo, Human Rights Watch imeangazia jinsi mwenendo wa vita vya Israel ulivyosababisha zaidi ya asilimia 90 ya watu wa Gaza kuyahama makazi yao.

Wakati huohuo vikosi vya Israel vinaendeleza mashambulizi ya anga katika maeneo yanayodhibitiwa na kundi la Hezbollah kwenye vitongoji vya mji mkuu wa Lebanon, Beirut. Mashambulizi hayo yameendelea kwa siku tatu mfululizo, eneo la kusini lilishambuliwa kwa mabomu.

Mzozo wa mashariki ya Kati | Lebanon
Mzozo wa Mashariki ya Kati: Mashambulizi kwenye mji wa BeirutPicha: Hassan Ammar/AP/dpa/picture alliance

Soma Pia:  Viongozi wa nchi za karabu watoa ujumbe mkali kwa Israel

Hata hivyo Israel pia imekabiliwa na hasara katika mashambulizi yake hayo ya ardhini dhidi ya Hezbollah baada ya wanajeshi wake sita kuuliwa katika mapigano karibu na mpaka wa nchi hizo mbili.

Vifo vyao vimefikisha iadadi ya wanajeshi 47 wa Israel ambao wameuawa katika mapigano na Hezbollah tangu Septemba 30.

Kwa upande wake Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limelaani mashambulizi ya wiki za hivi karibuni yaliyoulenga ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Lebanon, UNIFIL.

Wajumbe wamelaani mashambulizi ya mwezi Oktoba na mwezi wa Novemba ambapo maafisa kadhaa walijeruhiwa. Baraza la Usalama limezitolea mwito pande zote kuheshimu na kulinda usalama wa maafisa wa kikosi hicho pamoja na mali na miundombinu ya Umoja wa Mataifa.

Vyanzo: RTRE/AFP

 

 

Related Posts