Jeneza lenye mwili wa Mafuru lilivyoingizwa Karimjee

Dar es Salaam. Jeneza lenye mwili wa aliyekuwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Lawrence Mafuru limeingizwa kwenye viwanja vya Karimjee saa 6:02 mchana ikiwa ni saa 1:30 kupita tangu gari lenye mwili kuwasili kwenye eneo la viwanja hivyo saa 4:32 asubuhi.

Jeneza hilo, limeingizwa eneo maalumu na watu wanne waliokuwa wakisukuma kwenye kifaa mithili ya toroli, huku waombolezaji mbalimbali wakiwa wamesimama. Ni dakika chache kupita tangu Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipowasili viwanjani hapo.

Shughuli ya kuaga mwili wa Mafuru aliyefariki dunia Novemba 9, 2024 nchini India alipokuwa akipatiwa matibabu kwenye Hospitali ya Apollo, inafanyika leo Alhamisi Novemba 14, 2024 kwenye Viwanja vya Karimjee, jijini Dar es Salaam.

Jeneza lenye mwili wa Mafuru liliingizwa kwenye viwanja vya Karimjee likiwa linakokotwa kwenye gari maalumu cha kubeba jeneza, na dakika tano baadaye lilishushwa na kupelekwa eneo maalumu tayari kwa ibada kuendelea.

Awali, Mwili wa Mafuru uliwasili kwenye eneo la viwanja vya Karimjee saa 10:32 asubuhi, hata hivyo, baada ya jeneza lenye mwili wa Mafuru kuwasili, halikuingia moja kwa moja ndani ya viwanja hivyo.

Gari lililobeba jeneza lenye mwili huo lilipita kwenye lango kuu la kuingilia Karimjee na kwenda kupaki upande wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) hadi saa 6:02 mchana. Gari lenye mwili liliingia ndani ya viwanja vya Karimjee, ikiwa ni dakika tisa baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kufika saa 5:53 asubuhi.

Gari lililobeba mwili wa aliyekuwa katibu mtendaji wa Tume ya Mipango, Lawrence Mafuru likiwasili viwanja wa Karimjee jijini Dar es Salaam. Picha na Said Khamis

Mke wa marehemu, Noela Mafuru na watoto wake wawili ambao ni wasichana wakiwa na wanafamilia waliingia kwenye viwanja vya Karimjee saa 5:02 asubuhi kuungana na waombolezaji wengine ambao walisimama kuwapokea kisha kwenda kuketi eneo maalumu la familia na kusubiri kupokea jeneza lenye mwili wa mpendwa wao.

Wakati jeneza lenye mwili likiwa linasubiriwa kuingia uwanjani hapo ili kuendelea na ibada ya kuaga, salamu za rambirambi zilitolewa na viongozi mbalimbali huku baadhi wakimueleza namna ambavyo, mtaalamu huyo wa fedha na uchumi aliyehudumu katika sekta binafsi na umma alivyokuwa mpenzi wa soka na shabiki wa timu ya Yanga.

Wamemuelezea pia namna ambavyo alikuwa na furaha kupitiliza timu hiyo ilipoifunga moja ya timu mabao matano kwenye Ligi Kuu, jambo ambalo liliibua vicheko kwa waombolezaji.

Katika msimu uliopita wa 2023/24 ambayo Yanga iliumaliza kwa kutetea ubingwa, miongoni mwa timu zilizofungwa goli tano ni watani zake Simba. Mechi hiyo ilichezwa Novemba 6, 2023 katika dimba la Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Miongoni mwa viongozi waliojitokeza kuungana na familia na waombolezaji wengine ni Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda na wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama.

Wengine waliokuwepo ni Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, Naibu Spika wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mussa Zungu,  Balozi Ombeni Sefue, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila baadhi ya mawaziri, manaibu waziri na viongozi wengine.

Mwili wa Mafuru utazikwa kesho Ijumaa kwenye makaburi ya Kondo yaliyopo Tegeta jijini Dar es Salaam.

Nafasi ya Mafururu Kanisa la Waadvesta Wasabato

Wakati wengi wakimfahamu Lawrence Mafuru kama mtaalamu wa fedha na uchumi, katika dini pia alikuwa ni kiongozi wa kanisa.

Katika ibada ya kuaga mwili wake inayoongozwa na Askofu Mkuu wa Kanisa la Waadventista Wasabato (SDA), Jimbo la Kasikazini mwa Tanzania, Mchungaji Mark Malekana, amemtaja Mafuru kuwa enzi za uhai wake alihudumu kama mzee wa Kanisa la Magomeni SDA akihudumu kwenye nafasi hiyo kwa miaka mitatu.

Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari zaidi

Related Posts