Mambo manne turufu kwa Tanzania inaposhiriki G20

Dar es Salaam. Nishati safi ya kupikia, utunzaji wa mazingira, usalama wa chakula na diplomasia ya uchumi ni miongoni mwa maeneo muhimu ambayo Tanzania inatarajiwa kuyawekea msukumo inapokwenda kushiriki mkutano wa G20.

Mkutano huo unaozikutanisha nchi 20 zenye nguvu ya kiuchumi duniani utafanyika kuanzia Novemba 18 hadi 19, 2024 nchini Brazil na Rais Samia Suluhu Hassan amealikwa kuwa mmoja wa washiriki.

G20 ni mkutano unaofanyika kila mwaka, ukizihusisha nchi wanachama ambao ni Argentina, Australia, Brazil, Canada, China, Ufaransa, Ujerumani, India, Indonesia, Italia, Japan, Jamhuri ya Korea, Mexico, Russia, Saudi Arabia, Afrika Kusini, Uturuki, Uingereza na Marekani. Pia mashirika mawili ya kikanda, Umoja wa Ulaya na Umoja wa Afrika.

Nchi hizo zinachangia zaidi ya asilimia 85 ya pato la juu la dunia (GDP), huku zikiwa na asilimia 75 ya biashara ya kimataifa.

Kutokana na mwaliko alioupata Rais Samia kushiriki mkutano huo, wanazuoni wametaja mambo manne yanayohitaji kuwekewa msukumo na ndiyo yataibeba vyema Tanzania katika jukwaa hilo.

Mtaalamu wa nishati safi, Dk Manala Mbumba anasema ushiriki wa Tanzania katika mkutano huo ni fursa ya kuimarisha ajenda ya nishati safi ya kupikia.

Kwa mujibu wa mwanazuoni huyo wa Chuo Kikuu cha Usafirishaji (NIT), fursa hizo zitatokana na kupatikana kwa ufadhili wa miradi ya nishati safi ya kupikia.

“G20 inahusisha nchi zilizoendelea zenye uwezo mkubwa wa kifedha na teknolojia. Tanzania inaweza kuzungumza kuhusu changamoto na mahitaji yake katika nishati safi, ikilenga kufadhiliwa na mashirika ya kimataifa, benki za maendeleo au hata kupitia programu maalumu zinazofadhili miradi ya nishati safi,” anasema.

Anasema fursa nyingine inatokana na kuanzishwa kwa ushirikiano na kampuni za kimataifa kuhusu ajenda hiyo.

Dk Mbumba anasema ushiriki wa Tanzania utatoa jukwaa la kuvutia kampuni za kimataifa na wawekezaji wanaofanya kazi kwenye nishati safi ya kupikia.

“Hii ni fursa ya kuanzisha ubia wa kimkakati utakaosaidia kuleta teknolojia mpya ya kupikia inayopunguza matumizi ya kuni na mkaa, hali inayosaidia kuokoa mazingira,” anaeleza.

Uhamishaji wa teknolojia na maarifa ni fursa nyingine inayotajwa na mwanazuoni huyo kama turufu ya Tanzania kushiriki mkutano huo.

Anasema kuna uwezekano wa nchi kupata msaada katika uhamishaji wa teknolojia za kisasa kwa ajili ya matumizi ya nishati safi, kama majiko yenye ufanisi wa juu.

Ili kunufaika na fursa hizo, mtaalamu huyo anapendekeza mambo muhimu ambayo Tanzania inapaswa kuzungumza iwapo itapata fursa hiyo kuwa  ni athari za afya na mazingira kutokana na matumizi ya kuni na mkaa.

“Tanzania inaweza kuwasilisha hali ilivyo kwa sasa, ambapo matumizi ya kuni na mkaa yanachangia kwa kiasi kikubwa katika kuchafua hewa na kusababisha magonjwa ya njia ya upumuaji.”

“Jambo lingine ni uwezeshaji wa gharama nafuu kwa teknolojia safi ya kupikia. “Rais Samia anaweza kuomba kuanzishwa kwa mipango ya kusaidia nchi zinazoendelea kupata nishati safi kwa bei nafuu kwa sababu gharama za majiko safi na gesi asilia bado ni changamoto kwa watu wa kipato cha chini,” anasema.

Kwa mujibu wa Dk Mbumba, Tanzania isiache kuzungumza juu ya umuhimu wa kuunganisha nishati safi ya kupikia na malengo ya kijani ya kimataifa ili  kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa, kuokoa misitu na kuimarisha maisha ya watu wa vijijini.

“Ikiwa sehemu ya ajenda ya G20, Tanzania inaweza kuwa na nafasi ya kuonyesha umuhimu wa nishati safi kwa maendeleo endelevu,” anasema.

Hatua ya Tanzania kushiriki katika mkutano huo, anasema itaongeza uhamasishaji wa kimataifa kwa sekta ya nishati safi ya kupikia.

Anaeleza Tanzania itavutia miradi na rasilimali zinazolenga masuala ya afya, mazingira na maendeleo ya kiuchumi.

Mwanazuoni huyo anafungamanisha hamasa katika uwekezaji kwenye nishati safi ya kupikia na usalama wa chakula, ikiwa ni fursa nyingine ambayo Tanzania inaweza kunufaika nayo.

Anasema nishati safi ya kupikia inawezesha familia kupika vyakula vyenye lishe bora bila kuathiri mazingira au afya ya wapishi.

Kupitia ushiriki wa G20, anasisitiza Tanzania inaweza kusaidiwa kuimarisha juhudi za kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa, zinazoathiri upatikanaji wa chakula na afya za wananchi.

Dk Mbumba anasema kuna fursa lukuki na hata zile za kuboresha uzalishaji wa chakula kiasi cha kufanikiwa kuilisha Afrika na dunia kwa ujumla.

“Tanzania inaweza kutumia jukwaa la G20 si tu kuongeza uelewa kuhusu changamoto zake, bali pia kujiweka kwenye nafasi ya kuvutia msaada wa kifedha, kiufundi na kiteknolojia katika kuendeleza sekta ya nishati safi ya kupikia kwa ajili ya maendeleo endelevu ya nchi na afya ya wananchi wake,” anasema.

Mkutano huo kwa Tanzania ni fursa ya kujiweka sawa na kuimarisha mipango yake katika utunzaji wa mazingira, kama inavyoelezwa na Mhadhiri wa masuala ya mabadiliko ya tabianchi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Amos Majule.

Profesa Majule anasema Tanzania na Afrika imejipambanua kwa muda mrefu kukabili athari za mazingira, ingawa uhalisia wa kiuchumi unakuwa kikwazo wakati mwingine.

Anasema hata hatua ya Rais Samia kuwa kinara wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ni sehemu ya mikakati ya utunzaji wa mazingira.

Kwa sababu Rais Samia atakwenda kushiriki mkutano wa G20, anasema ni fursa kwa Tanzania kuweka msukumo wa mataifa hayo yaliyoendelea yawezeshe misaada ya kifedha kwa nchi zinazoendelea kujenga uhimilivu wa mazingira.

“Wachafuzi wa mazingira siyo sisi, ni hizo nchi zilizoendelea kupitia miradi yao ya uwekezaji. Tanzania tunapokwenda kushiriki mkutano huo ni fursa ya kuwasisitiza watuwezeshe kukabili athari zinazojitokeza,” anasema.

Uwezeshaji na ufadhili huo, Profesa Majule anasema unapaswa kufanyika hata kwenye upatikanaji wa majiko nafuu kwa ajili ya wananchi kupika kwa nishati safi.

Pia anapendekeza Umoja wa Ulaya (EU) ambaye ni mmoja wa wanachama wa G20, aongeze ufadhili wa elimu kuhusu mazingira kwa wasomi wa Afrika.

“Kwa sasa EU anatoa ufadhili lakini kiu yetu aongeze zaidi ili kunufaisha wengi. Kwa hiyo jopo litakalokwenda bila shaka litayaeleza hayo,” anasema.

Kwa kuwa mkutano huo unayakutanisha mataifa yenye nguvu kiuchumi, ushiriki wa Tanzania utatoa fursa ya kujitangaza kama inavyoelezwa na Mhadhiri wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Benedict Mongula.

Profesa Mongula anasema watakaokwenda wanapaswa kuhakikisha wanatumia nafasi hiyo kutangaza fursa za uwekezaji na utalii zinazopatikana nchini.

“Kampuni, mashirika na viongozi wa nchi za G20 wataijua Tanzania kupitia ushiriki wake. Si kila mtu anaijua Tanzania, tunapokwenda tumejieleza vizuri tutajulikana na kuvuna fursa,” anasema.

Profesa Mongula anaeleza msingi wa uchumi wa taifa lolote ni uwekezaji, hivyo kuna fursa ya kuwavutia wawekezaji kutoka G20.

Anauhusisha ushiriki wa Tanzania katika mkutano huo na nafasi ya nchi kuepuka matendo yasiyofaa ulimwenguni.

“Inatusaidia kwa sababu hata matatizo yetu ya ndani tutaona aibu kwa sababu tutaona Jumuiya ya Kimataifa itatuona vibaya.

“Tusiende kienyeji tujiandae ili kuonyesha fursa zetu, waende watu wanaotakiwa watakaotumia vema fursa zitakazopatikana,” anasema.

Related Posts