Dar es Salaam. Teknolojia ya kuzalisha bidhaa bora, mtaji na soko hususani la kimataifa vimetajwa kuendelea kuwa changamoto kwa wajasiriamali na wafanyabishara nchini Tanzania.
Kundi hilo limetajwa kukwamishwa na mtaji kwaajili ya kukuza viwanda vyao, kununua teknolojia mpya, kuongeza ajira na vipato kwenye viwanda ili kuweza kuzalisha bidhaa bora.
Hayo yamebainishwa na Meneja wa Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (Sido) mkoa wa Dar es Salaam, Hopeness Elia alipozungumza na waandishi wa habari wakati wa warsha fupi iliyowakutanisha wafanyabiashara na wajasiriamali na wadau wa maendeleo walioingia ubia na kundi hilo, Benki ya Maendeleo ya TIB.
Warsha hiyo imehudhuriwa na wafanyabiashara wapatao arobaini kutoka sekta mbalimbali ikiwemo viwanda, kilimo, ujenzi, usafirishaji wa bidhaa nje, na afya katika makao makuu ya Sido jijini Dar es Salaam leo Novemba 14, 2024.
Elia amesema katika kutatua hilo ndio maana wamewaita wajasiriamali kukutana na wadau hao wa maendeleo kuangalia namna ya kutatua changamoto hizo
“Teknolojia zinazotumika zinatoa bidhaa hafifu tunawasaidia wapate kununua teknolojia za kisasa zinazozalisha bidhaa bora zipate soko kwenye soko la dunia,” amesema.
Ameongeza changamoto nyingine ni kwenye mikopo kwani inayotolewa kwao inariba kubwa na sababu ya riba kubwa hailipiki ni mikopo chechefu sasa mikopo mingi ikiwa chechefu riba inakuwa kubwa.
“Japo Sido tumejitahidi tunamikopo ya asilimia tisa hadi 13 na tunatoka kati ya Sh1 hadi 500 milioni lakini bado ulipaji wake sio mzuri hivyo inaleta ugumu kuleta riba zaidi,” amesema.
Kufuatia hali hiyo amefafanua kinachofanyika wanatoa elimu kwa kurudia rudia kwa kundi hilo waweze kuelewa aidha wanatoa njia za masoko, mitaji na teknolojia ingawa mwendo ni mdogo.
“Tunawatembelea maeneo wanayozalishia bidhaa zao na maeneo yao ya biashara, tunatengeneza kanzidata ya wajasiriamali wadogo na wakati. Kuweza kuwapata kwa haraka.”
Amesema wanawaalika kwenye maonesho waweze kujifunza kwa wengine waweze kukua zaidi huku msingi ikiwa kuwatatulia changamoto zinazowakabili.
“Ndio maana tumewaita TIB wakutane nao waweze kuona namna ya kupatia ufumbuzi wa changamoto ya mitaji,” amesema.
Amesema pia eneo lingine ni soko viwanda vingi vinazalisha bidhaa wanashindwa kufikia sokoni kwa bei nzuri. Huku akisisitiza kwamba wamealika watu wanaouza nje ya Tanzania kuona watafikiaje soko la Afrika, Ulaya na hata Amerika.
Amesema Sido wanahudumia wajasiriamali kuanzia wadogo na wanawalea kuanzia kuwatembelea na wengine wako nao kwaajili ya kuwakuza.
Kwa upande wake, mwakilishi wa meneja wa Benki ya Maendeleo ya TIB kanda ya Dar es Salaam, Eugene Ingwe amesema azma yao ni kuwainua wajasiriamali kuendelea kuimarisha uchumi wao na taifa kwa ujumla.
Ingwe amesema mikakati waliyonayo kupunguza mikopo chechefu ni kufanya upembuzi yakinifu kwa wateja na kuchakata mikopo yao ili kufuata vigezo vinavyohitajika kibenki.
“Tunawapatia wajasirimali na wafanyabiashara wa Kitanzania kwa kuwapa mikopo kwa nyakati zote,” amesema Ingwe.
Mmoja ya wajasiriamali Irene Simon amesema changamoto nyingine inayowakabili ni uwepo wa vibali vingi vinavyotakiwa ambavyo ni gharama na vinachukua muda kupata.
“Mitaji ya kusaidia biashara uweze kukua ni changamoto sana kupata masharti ni mengi sana” amesema Irene.
Mjasiriamali Flotea Massawe, mkurugenzi wa kampuni ya uchakati vyakula vya virutubisho ya Ajabu Enterprises amesema Sido inapaswa kuendelea kutoa elimu kwa wajasiriamali ili wazalishe bidhaa zinazohitajika sokoni ili kuzidi kushindana.
Aidha, Fred Swai, Mkurugenzi Mtendaji wa Miombo GR Limited amesema Sido wakiwekeza nguvu hata lengo la Serikali kuwa na Tanzania ya viwanda litafikia na litakaa mahali pake.
Amesema suala la riba linapaswa kuwa nafuu na mikopo ikiwa inakuja kwa wakati itawezesha wao kufanya kazi inavyotakiwa.