Mchango wa huduma za miamala katika uchumi

Dar es Salaam. Wakati takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA) zikionyesha ongezeko la matumizi ya huduma za miamala ya simu hadi kufikia akaunti milioni 60.8 (Septemba, 2024) wachambuzi wanaeleza kuwa idadi hiyo ni zaidi ya ongezeko.

Akizungumzia nafasi ya huduma za miamala ya simu katika kuinua watu kiuchumi, Mchambuzi wa masuala ya fedha, Rashid Aziz alisema huduma za fedha kwa simu zimeongeza ujumuishi wa huduma za kifedha katika maeneo mengi ambayo pengine hadi sasa yangekuwa hayajafikiwa.

“Huduma za mikopo zimesogezwa karibu zaidi na watu, utunzaji wa akiba na hata utumaji na upokeaji wa fedha sasa umerahisishwa,” alisema Aziz.

Alisema kwa huduma hizo kufika maeneo mengine kumeongeza usalama wa kifedha ambao unaimarisha uchumi wa mtu mmojammoja, maana hata aina ya wizi sasa imebadilika.

“Tofauti na zamani, mtu hivi sasa akitaka kukuibia inabidi awe na Password (nywila) yako, siyo rahisi tena kama zamani,” alisema Aziz na kuongeza kuwa huduma za miamala kwa njia ya simu zimeongeza hata mzunguko wa fedha.

Aidha, Aziz aliongeza kuwa urahisi unakuwa si tu kwa watumiaji, bali hata kwa Serikali kudhibiti mfumo wa fedha, kwani wakati wote wanaweza kujua kiasi cha fedha kilichopo kwenye mzunguko.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya huduma za simu Vodacom Tanzania, ambayo inaongoza kwa kuwa na watumiaji wengi wa huduma za miamala ya simu, Philip Besiimire alisema mbali na huduma za miamala, kampuni hiyo hutoa elimu na ujuzi ili kuwa na uendelevu.

“Tunashirikiana na wadau kutoa mafunzo ya msingi ya akiba kupitia wataalamu wa fedha waliobobea, tumewawezesha na kuwapa ujuzi zaidi ya makundi 12,000 katika masuala ya uwekaji wa akiba ndogondogo,” alisema Besiimire, ambaye kampuni yake inaongoza soko kwa asilimia 36.9.

Besiimire alisema kupitia huduma yao ya M-Koba (huduma za kutunza akiba inayotolewa na M-pesa) kampuni anayoiongoza imefanikiwa kuvutia makundi na wateja zaidi, huku ikichangia kwa kiasi kikubwa uwezeshaji wa kifedha kwa wanawake.

“Wanawake ni zaidi ya asilimia 50 ya wateja wetu wa M-Koba na wanafanya zaidi ya asilimia 60 ya thamani ya jumla ya miamala yote ya M-Koba, yenye thamani ya Sh1 trilioni kwa mwaka,” alisema Besiimire katika taarifa ya kampuni hiyo iliyotolewa mapema mwezi huu.

Kiongozi huyo alisema Vodacom itaendelea kuwawezesha wateja wake, hususan katika safari ya kuelekea ulimwengu wa kidijitali ambako wanaweza kufikia fursa zitakazoboresha maisha yao kijamii na kiuchumi.

“Ili kufanikisha hili, ongezeko la matumizi ya simu za kisasa ni muhimu, na tutashiriki kikamilifu katika kukuza matumizi ya simu za kisasa kupitia ushirikiano ili kuongeza upatikanaji na kuboresha ufanisi wa gharama,” alisema.

Related Posts