Mkutano wa COP29 waghubikwa na joto la kidiplomasia – DW – 14.11.2024

Wakati wajumbe katika mazungumzo ya COP29 wanaendeleza harakati za kufikia makubaliano ya ufadhili, mazungumzo hayo sasa yameghubikwa kwa kiasi kikubwa na mzozo wa kidiplomasia.

Waziri wa mazingira wa Ufaransa afutilia mbali safari ya Baku

Siku ya Jumatano, Pannier-Runacher, alisema hatosafiri kuelekea Baku baada ya Rais wa Azerbaijan Ilham Aliyev kuishutumu Ufaransa kwa kile alichokiita “uhalifu” wa kikoloni na “ukiukaji wa haki za binadamu” katika maeneo yake ya ng’ambo.

Pannier-Runacher asema hotuba ya Rais Aliyev haikubaliki

Pannier-Runacher alisema hotuba hiyo haikubaliki na kwamba ni ya hadhi ya chini kwa urais wa COP.  Waziri huyo pia ameongeza kuwa matamshi ya Rais Aliyev ni ”ukiukwaji mkubwa wa kanuni za maadili” za mazungumzo hayo ya Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya hewa.

Tofauti zaibuka katika mkutano wa COP29

Akijaribu kutuliza hali hiyo hii leo, mwakilishi mkuu wa Azerbaijan katika mazungumzo hayo ya COP29 Yalchin Rafiyev, amesisitiza kuwa nchi yake imewezesha kuwepo kwa machakato jumuishi na kwamba wamefungua milango yao kwa kila mtu kushiriki katika mazungumzo yenye tija.

Rais wa Azerbaijan Ilham Aliyev akizungumza katika kongamano la kimataifa la wanahabari huko Shusha, Azerbaijna mnamo Julai 21,2023
Rais wa Azerbaijan Ilham AliyevPicha: Bulkin Sergey/Russian Look/IMAGO Images

Umoja wa Ulaya leo umetaja mashambulizi hayo ya maneno kutoka kwa Rais Aliyev dhidi ya nchi za Umoja huo za Ufaransa na Uholanzi kama yasiokubalika na yanayotishia kuhujumu kongamano hilo la mazingira linaloendelea mjini Baku.

Ufaransa, Kenya na Barbados zaamini mapato zaidi kutoka kwa kodi

Katika hatua nyingine, Ufaransa, Kenya na Barbados zinaamini kwamba mamia ya mabilioni ya dola yanaweza kupatikana kutoka kwa kodi za mshikamano wa kimataifa dhidi ya viwanda vinavyochangia zaidi uchafuzi wa mazingira ili kusaidia mataifa yanayoendelea.

UN: Mataifa tajiri duniani yanastahili kutoa zaidi ya mara mbili fedha za tabia nchi

Waziri mkuu wa Barbados Mia Mottley, mwanaharakati mkuu wa hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, ameuambia mkutano huo wa COP29 mjini Baku kwamba wakati umewadia wa kuzingatia kodi hizo.

Takriban dola bilioni 350 zaweza kukusanywa kwa mwaka

Mottley amesisitiza kuwa kati ya nishati inayotumika kwenye safari za baharini, kwenye mashirika ya ndege na ile ya visukuku, kuna uwezekano wa kukusanya takriban dola bilioni 350 kwa mwaka .

COP29: Mataifa masikini yapewe fedha zaidi

Ripoti ya jopo kazi hilo iliyotolewa huko Baku, pia imesema sehemu kubwa za uchumi pia zinachafua mazingira lakini zina mchango mdogo kwa fedha za umma, maendeleo na hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

 

Related Posts