Mwanafunzi aliyepotea siku 26 mlimani Babati kuhamishwa shule

Arusha. Familia ya mwanafunzi Joel Johannes (14), aliyepotea kwa siku 26 akiwa na wanafunzi wenzake waliopanda Mlima Kwaraa, mkoani Manyara kwa ajili ya ziara ya mafunzo, imesema itamhamisha shule mtoto huyo ili wakae naye karibu.

Aidha familia hiyo imesema mtoto huyo alipelekwa Hospitali ya Taifa ya akili (Mirembe) mkoani Dodoma kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo  Alhamisi Novemba 14, 2024 kuhusu maendeleo ya mtoto huyo, baba mzazi, Johannes Mariki amesema kwa sasa mtoto wao anaendelea vizuri na ameruhusiwa kutoka Hospitalini Milembe alikokuwa kwa siku kadhaa kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

Joel ambaye anasoma kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Bagara, alitoweka tangu Septemba 14, 2024 na kupatikana Oktoba 9, 2024 wilayani Babati mkoani humo.

“Tunamshukuru Mungu mtoto anaendelea vizuri kwa sasa na ameruhusiwa kutoka hospitali alikolazwa Dodoma alikopelekwa na serikali kwa ajili ya uchunguzi wa afya ya akili, tutamrudisha kliniki tena Novemba 21, 2024,” amesema Mariki.

Kuhusu shule, mzazi huyo amesema kwa sasa hawatamrudisha kwenye ile shule bali wanamtafutia shule iliyokaribu kusudi wakae naye jirani.

“Alikuwa kidato cha pili na hajaweza kufanya mitihani, pale shuleni hatutaki asome tena, tutamhamisha asisome mbali na sisi, tunataka tukae naye karibu zaidi. Hapo kuendelea na shule labda mwakani tena, tunasubri tuone kama atakubaliwa kuendelea au atatakiwa kurudia kidato cha pili,” amesema mzazi huyo.

Awali, Joel alilazwa kwa siku kadhaa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara na Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dk  Catherine Magali alisema walimpokea mwanafunzi huyo akiwa amedhoofu.

Awali Septemba 14, 2024, akizungumzia kupotea kwa mwanafunzi huyo, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Babati, Simon Mdee alisema safari hiyo ya masoko kwa wanafunzi hao ilihusisha wanafunzi 103, wakiwa na walimu na waongozaji wapanda mlima.

Related Posts