MWENENDO WA SEKTA YA MADINI NCHINI

*Mchango wa Sekta ya Madini kwenye Fedha za Kigeni*
Sekta ya Madini imeendelea kukua siku hadi siku ambapo katika Mwaka wa Fedha2022/23 ilikuwa Sekta kinara kwa kuchangia zaidi ya asilimia 56 kutokana na mauzo ya bidhaa za madini nje ya nchi.

*Mchango wa Sekta ya Madini kwa kodi za ndani*
Sekta ya Madini ilichangia asilimia 15 ya kodi za ndani zinazotokana na shughuli za madini ambazo ni sawa na shilingi trilioni 2.1.

*Mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa*
Mwaka 2023, Sekta ya Madini ilichangia asilimia 9.0 kutoka asilimia 7.2 mwaka 2022. Lengo la Serikali ni Sekta ya Madini kuchangia asilimia 10 katika Pato la Taifa ifikapo mwaka 2025.

*Habari Njema kwa Wachimbaji Wadogo*
Mwishoni mwa mwezi huu, mitambo mingine 10 ya uchorongaji kupitia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) inafika kwa ajili ya shughuliza uchorongaji madini. Gharama za uchorongaji ni kubwa lakini Serikali inakwenda kubeba baadhi ya gharama na mchimbaji atatakiwa kulipia shilingi milioni 10 badala ya milioni 25.

*Mazingira Rafiki ya Uwekezaji Sekta ya Madini Kuirejesha kampuni kubwa ya Madini Duniani BHP*
BHP ni kampuni kubwa ya madini kutoka nchini Australia ambayo kwa kipindi cha miaka 15 iliyopita ilifunga shughuli zake Barani Afrika na sasa wanafikiria kurejea Tanzania. Hii ni heshima kubwa kwetu kama taifa kwasababu wameona ni sehemu salama kufanya uwekezaji wao.

*Mchango wa Sekta ya Madini kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali*
Habari kubwa ni kwamba, ndani ya siku 121, tayari tumekusanya shilingi bilioni 370 katika Mwaka huu wa Fedha 2024/25 kuanzia mwezi Julai, 2024.

*Udhibiti wa Biashara ya Madini*
Tumeimarisha udhibiti wa utoroshaji madini kwa kuanzisha masoko ya madini ambapo hadi sasa tuna jumla ya masoko 43 na vituo vya ununuzi 105. Kupitia masoko hayo, biashara ya madini yenye thamani ya shilingi trilioni 4 na bilioni 700 zilikusanywa kupitia tozo mbalimbali. Hali hii inaonesha kuwa tumeimarisha udhibiti kwenye eneo hili.

*Kiwanda cha Kusafisha Metali- Taifa litakuwa na uwezo wa kuzalisha bidhaa za mwisho*
Hekta zipatazo 1,331 tayari zimetengwa kwa ajili ya mradi wa kusafisha madini ya metali katika eneo la Mgodi wa Buzwagi, Kahama- Shinyanga, mradi huu unatarajia kutumia dola za Marekani milioni 500 na kitakuwa na uwezo wa kuzalisha bidhaa za mwisho. Mbali na kiwanda hicho, pia kutakuwa naviwanda vingine kwenye viwanda vingine kwenye mnyororo wa shughuli za madini.

*Pongezi kwa Wachimbaji Wakubwa, wa Kati na Wadogo*
Ninawapongeza wachimbaji wakubwa, wa kati na wadogo kutokana na mchango wao kwa maendeleo na ukuaji wa sekta yetu. Kwa wachimbaji wadogo, sekta hii ndogo imekuwa mfano kwa mataifa mengi katika nchi za Kusini mwa Afrika (SADC). Hivi sasa sekta hii ndogo inachangia asilimia 40 ya maduhuli ya Serikali.

*Biashara ya Almasi duniani*
Miezi miwili iliyopita nilikuwa katika Mgodi wa Almasi Mwadui, sababu iliyopelekea soko la almasi kushuka ni kwasababu ya uwepo wa almasi zinazozalishwa maabara. Hivi sasa dunia inapambana na almasi za maabara. Kwa upande wetu, wachimbaji wanaendelea na shughuli zao.

*KWANINI MKUTANO WA KIMATAIFA WA UWEKEZAJI SEKTA YA MADINI TANZANIA*

*Kuvutia Uwekezaji*
Mkutano wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini unalenga kuimarisha mazingira ya uwekezaji, kuendelea kuvutia wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi na kutumika kama jukwaa la kujadili kwa pamoja mustakabali wa sekta ya madini, kushirikishana maarifa, ujuzi, uzoefu na kuangazia fursa mpya zinazojitokeza katika sekta hii inayokua kwa kasi.

*Nafasi ya wadau kujifunza Sera, Sheria, Mikakati mipya ya Serikali*
Unatoa nafasi kwa washiriki kujifunza kuhusu Sera na mikakati mipya ya serikali, kujadili masuala ya kisheria na kiuchumi yanayohusiana na madini, na kushuhudia teknolojia mpya na ubunifu unaoweza kuleta thamani zaidi katika utafiti, uchimbaji na uongezaji thamani wa madini.

*Ushirikiano thabiti*
Mkutano huu unalenga si tu kuvutia uwekezaji, bali pia kuweka msingi thabiti wa ushirikiano baina ya wadau, kuimarisha uzalishaji wa madini, na kuhakikisha kuwa rasilimali hizi zinawanufaisha Watanzania kiuchumi, kijamii na wawekezaji

*Watoa Mada*
Mkutano utakuwa na jumla ya mada 8 utawakutanisha watoa mada wapatao 20 kutoka nje ya nchi na 37 kutoka nchini waliobobea kwenye sekta ya madini.

*Washiriki wa Mkutano*
Mkutano utawashiriki wadau wapatao 1,500 kutoka ndani na nje ya Tanzania, ukiwahusisha Mawaziri wa Madini kutoka nchi nyingine za Afrika, Watendaji Wakuu wa kampuni kubwa za madini duniani zilizowekeza na zinazotarajia kuwekeza nchini; watafiti; mabalozi 31 wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini; mabalozi wanaoiwakilisha nchi yetu nje ya nchi akiwemo Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Umoja wa Mataifa, Mhe. Balozi Hussein Kattanga; mashirika ya kimataifa; waongezaji thamani madini; wafanyabiashara; taasisi za fedha; vyuo Vikuu vya kati taasisi za umma na binafsi zinazojihusisha na shughuli za madini, viongozi mbalimbali wa kitaifa kutoka wizara, taasisi, mikoa,halmashauri na idara za Serikali.

*Kaulimbiu ya Mkutano wa Mwaka 2024*
Mkutano wa Mwaka huu unaoongozwa na kaulimbiu Uongezaji thamani Madini kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii, inayolenga kuhimiza umuhimu wa uongezaji thamani wa madini kama njia ya kuleta faida za kiuchumi na kijamii kwa maendeleo endelevu ya taifa letu na dunia; kupandisha thamani ya madini yanayozalishwa nchini kabla ya kusafirishwa nje kwa lengo la kuchochea uanzishwaji viwanda vitakavyokuwa na manufaa nchini, kwa majirani wanaotuzunguka na duniani.

*Hafla ya Usiku wa Madini*
Mkutano huu utaambatana na hafla ya usiku wa madini tukio maalum la kutambua mchango wa wadau waliofanya vizuri katika sekta ya madini kupitia makundi mbalimbali. Pia, utaambatanana onesho la bidhaa za madini ya vito na madini mengine yakiwemo ya viwandani na ujenzi kwa lengo la lengo la kuonesha fursa zilizopo na kutambua matumizi ya madini katika maisha ya kila siku ya kiuchumi na kijamii.

*Ufunguzi, Kufunga Mkutano*
Mkutano wa 6 wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini Tanzania utafunguliwa rasmi tarehe 19 Novemba, 2024 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassa, utafungwa tarehe 21 Novemba, 2024 na Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi tarehe 21 Novemba, 2024.

*#TMIC2024*

*#ValueAdditionforSocio-economicDevelopment*

*#InvestInTanzaniaMiningSector*

*#UongezajithamaniMadinikwaMaendeleoyaKiuchuminaKijamii*

Related Posts