KOCHA wa zamani wa Yanga ambaye kwa sasa anaifundisha Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini, Nasredine Nabi amekumbwa na balaa baada ya kuumia goti na kulazimika kufanyiwa upasuaji.
Kocha huyo aliyewahi kuifikisha Yanga fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, amefanyia upasuaji huo baada ya kuumia goti la mguu wa kushoto akiwa mazoezini wakati akijaribu kuwaelekeza jambo wachezaji wake.
Nabi anayeisuka timu yake mpya aliyoungana nayo msimu huu akitokea FAR Rabat ya Morocco, aliwahishwa hospitali na kufanyiwa upasuaji wa haraka jana asubuhi baada ya kuhisi maumivu makali.
“Kuna kitu nilikuwa najaribu kuwaelekeza wachezaji wangu tukiwa mazoezini, nilipopiga mpira na kuurudisha nilipata maumivu makali sana,” amesema Nabi na kuongeza.
“Hata madaktari wa timu waliponisaidia bado nilipata maumivu, nikapelekwa hospitali na kufanyiwa upasuaji, uliokwenda vizuri na nimetoka hospitali, leo nipo nyumbani.”
Kocha huyo aliyebeba mataji mawili ya Ligi Kuu Bara akiwa na Yanga, atakuwa nje kwa muda wa wiki mbili akimuachia msaidizi wake Cedric Kaze kuendelea kukinoa kikosi hicho.