Unguja. Katika kupambana na janga la ogezeko la ajali za barabarani, Zanzibar imeendelea kubuni mikakati, safari hii kwa mara ya kwanza itaanza kuadhimisha wiki ya usalama barabarani ambayo itatumika kutoa elimu kwa watumiaji wa barabara.
Akizungumza kuhusu wiki hiyo Novemba 14, 2024 Waziri wa Ujenzi, Mawasilinano na Uchukuzi, Dk Khalid Salum Mohamed amesema licha ya juhudi ambazo zimekuwa zikichukuliwa za kudhibiti usalama wa watumiaji wa barabara bado zinaendelea kuwa tishio na kugharimu maisha ya wengi.
“Tumejipanga kuhakikisha tunafanya vizuri wiki hiyo licha ya kuwa Zanzibar ni kwa mara ya kwanza kufanya jambo hili lakini kwa kuwa ni kupunguza ajali tunaamini tutafanya vizuri,” amesema.
Kwa Mujibu wa Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar (OCGS) kwa mwaka 2023, watu 385 wamepoteza maisha katika ajali 193 zilizoripotiwa. Kati ya hao, 343 walikuwa wanaume na 42 ni wanawake.
Idadi hiyo ni ongezeko la asilimia 19.2 kutoka watu 323 waliofariki dunia mwaka 2022.
Majeruhi wameongezeka kwa asilimia 12.5 kutoka 136 mwaka 2022 hadi kufikia 153 mwaka 2023. Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, Zanzibar ina watu 1.8 milioni.
Kwa mujibu wa OCGS, waathirika 151 (waliofariki na kujeruhiwa) walikuwa abiria, wapanda baiskeli na pikipiki walikuwa 130 na waenda kwa miguu 78, huku madereva walikuwa 26.
Imeelezwa makosa 38,598 yameripotiwa, kati ya hayo 38,522 yameripotiwa kwa wanaume na 76 kwa wanawake.
Kosa kubwa lililoripotiwa ni kutofuata miongozo na kanuni za usalama barabarani makosa yakiwa 12,419.
Dk Khalid amesema lengo kuu la maadhimisho haya ni kuendelea kutoa elimu ya matumizi sahihi ya barabara na kuwaamsha wananchi juu ya janga la ajali za barabarani linaloendelea kuiumiza Zanzibar katika jambo hilo.
Kaulimbiu ya maadhimisho hayo yatakayoanza Novemba 16 hadi 23, 2024 inasema ‘Utekelezaji wa mkakati wa usalama barabarani Zanzibar 2024-2030 ni suluhisho la ajali za barabarani.’
“Katika kipindi chote cha maadhimisho ya wiki ya usalama barabarani kutakuwa na shughuli mbalimbali zinazofanyika zikiwemo kongamano, usafi wa mazingira, kutoa elimu juu ya matumizi sahihi ya barabara na uchangiaji wa damu kwa hiari,” amesema.
Pia, kutakuwa na maonyesho katika viwanja vya Kisonge Mnarani ambayo yatajumuisha taasisi za Serikali na binafsi.
Omar Said, mdau wa masuala ya barabarani amesema bado elimu kubwa inahitajika kwani kuna uzembe unaofanywa na madereva bila kuzingatia alama za barabarani wala kujali wapitinjia.
Kwa mujibu wa mkataba wa usalama barabarani barani Afrika nchi wanachama zinatakiwa kuunda mabaraza ya usalama ambayo yataratibu shughuli za usalama barabarani katika nchi husika kwa kuzingatia sheria namba 10 ya mwaka 2019 ya Sheria ya Usafiri Barabarani pamoja na marekebisho yake.