Mwanza. Ugonjwa wa pumu ya ngozi unatajwa kuwa kinara wa magonjwa ya ngozi yanayowatesa wakazi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Takwimu zinaonyesha wastani wa wagonjwa wapya 300 wanaogundulika kuugua na kutibiwa magonjwa ya ngozi katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando kila wiki, wagonjwa 120 sawa na asilimia 40 hugundulika kuugua ugonjwa huo.
Takwimu hizo zimetolewa leo Alhamisi Novemba 14, 2024 na Mkuu wa Idara ya Ngozi Bugando, Dk Nelly Mwageni wakati wa upimaji wa magonjwa ya ngozi kwa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT) Mwanza na jamii inayokizunguka chuo hicho.
Dk Mwageni amesema hata kwenye kambi hiyo ambayo iliyohudumia watu 302 wote wakibainika kuugua maambukizi ya ngozi, zaidi ya watu 100 sawa na asilimia 30 wamegundulika kuugua ugonjwa huo na wengine wakikutwa na maambukizi ya fangasi za kichwani, mba, vibarango na mapunye.
“Ugonjwa huu unawatesa sana watoto chini ya miaka 18 na vijana wenye umri wakati na mara nyingi wanafika hospitalini wakilalamika ngozi kuwasha, hivyo hujikuna kupita kiasi. Wengi wao wanakimbilia hospitalini ili kupatiwa msaada wa haraka wa miwasho,” amesema Dk Mwageni.
Kuhusu kisababishi, Dk Mwageni amesema ugonjwa husababishwa na kurithi na mabadiliko ya mazingira yanayoweza kusababisha bakteria wa ngozi kujibadili na kuanza kushambulia ngozi ya mwili.
Mtaalamu huyo wa ngozi amesema mbali na pumu ya ngozi, wakazi wa kanda hiyo pia wanasumbuliwa na maambuziki ya fangasi za kichwa na kucha kutokana na matumizi holela ya vipodozi sambamba na fangasi zinazoshambulia seli za nywele, jambo linalosababisha zisiote kwa mpangilio.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Ngozi na zinaa hospitali ya Bugando, Jacqueline Iraba amesema magonjwa ya ngozi ni miongoni mwa changamoto inayowatesa wanaume katika kanda hiyo huku akitaja ugonjwa wa ‘Alopecia’ kuwa hushambulia mizizi ya nywele na kuwasababisha kipara.
“Kuna magonjwa mengine ya nywele yanashambulia mzizi wa nywele na kufanya zisiote ambapo asilimia kubwa ya jamii huwa wanahisi ni kurogwa kwamba nililala usiku nikanyolewa asubuhi nikaamka sina nywele lakini siyo kurogwa ni ugonjwa nywele zimeshambuliwa hazioti.
“Tunashauri wenye tatizo hilo wasikimbilie kwenda kwa waganga wa kienyeji ama kutumia mitishamba kutafuta mchawi wake badala yake aje Bugando tupo kwa ajili ya kumhudumia,” amesema Dk Iraba.
Wakati wataalam hao wakitahadharisha juu ya matumizi holela ya vipodozi na magonjwa hayo, Naibu Waziri wa Afya Serikali ya Wanafunzi chuoni hapo (Sautso), Rahma Omary amewataka wanafunzi na jamii kuongeza umakini na kuepuka matumizi holela ya vipodozi ambavyo vinaweza kugeuka kemikali na kuathiri ngozi.
“Ukiangalia katika mitandao kuna dawa ambayo yanatangazwa kwamba tumia dawa flani kuongeza maumbile sehemu flani, Sautso tunaomba sana wanafunzi wakae mbali na matumizi holela ya dawa hizo. Kama una shida ya kutumia vipodozi ama dawa nenda katafute ushauri kwa wataalam,” amesema Rahma.
Mwanafunzi wa Shahada ya Sheria SAUT, Stella Mwilanga ametaja ulimbukeni kuwa moja ya sababu zinazochochea vijana kujiingiza katika matumizi holela ya vipodozi na dawa zinazoweza kuwasababisha madhara kwenye ngozi na kiafya.
Mwanafunzi mwingine, Mwita Chacha ameomba taasisi za afya kuendelea kutoa elimu kwa Umma kuhusiana na athari za matumizi holela ya vipodozi na dawa zinazosababisha maambukizi ya ngozi kama kilichofanywa na Bugando chuoni hapo.
Bugando ambayo ni hospitali inayohudumia wakazi zaidi ya milioni 12 wa kanda hiyo imeendesha kambi hiyo ikiwa ni maadhimisho ya siku ya kimataifa ya magonjwa ya ngozi duniani kwa kutoa huduma ya ushauri na uchunguzi wa magonjwa ya ngozi, nywele na kucha bila malipo.