Wakati wa jukwaa la uzinduaji lililoandaliwa na Taasisi ya Hakirasilimali mapema mwezi huu, Waziri wa Madini, Antony Mavunde alisema kuwa Tanzania imeandaa mkakati maalumu wa kuyavuna madini mkakati ambao utaifanya nchi kuwa kinara wa uzalishaji wa madini hayo duniani.
Alisema Tanzania inashika nafasi ya tatu Afrika katika uzalishaji wa madini ya kimkakati ya kinywe, ikitanguliwa na Madagascar na Msumbiji hivyo kuna haja ya kuongeza nguvu ya uzalishaji kuongoza kwa kuwa mzalishaji mkubwa zaidi barani Afrika.
“Tanzania inashika nafasi ya tatu, ikizalisha asilimia 0.64 ya mahitaji yote duniani, ikitanguliwa na Madagascar na Msumbiji,” alisema Mavunde na kuongeza kuwa rekodi hiyo imewekwa na mzalishaji mdogo God Mwanga, aliyepo eneo la Kwa Msisi, wilayani Handeni, Mkoa wa Tanga.
“Kuna leseni 12 hazijaanza kufanya kazi, zikianza kufanya kazi hizi Tanzania itakuwa kinara wa uzalishaji madini ya kinywe (graphite) ya barani Afrika, ” aliongeza Waziri huyo, mwenye dhamana ya madini na shughuli zake hapa nchini.
Hata hivyo, pamoja na mipango na matamanio hayo, swali linabaki kuwa ni namna gani maono hayo kuwa uhalisi kwa kuzingatia mazingira tofauti ya ndani na nje ya nchi.
Tafiti nyingi zinaonyesha kuwa kutokana na uhitaji wa madini hayo duniani, nchi zenye akiba kubwa zinaweza kupata manufaa makubwa ya kiuchumi lakini hilo litategemea usimamizi mzuri na mbinu zitakazotumika.
Mtaalamu wa sera na maendeleo wa Jukwaa la mtandao wa madeni na maendeleo (Afrodad) John Oduk ameshauri kuwa mataifa ya Afrika yenye utajiri wa madini ya kimkakati, ikiwemo Tanzania yanapaswa kuunganisha nguvu ili kufanikisha safari ya muhamo wa kutumia nishati safi.
Anasema ili nchi za Afrika zifikie uzalishaji mdogo wa hewa ya kaboni, hazina budi kuweka nguvu ya pamoja katika madini ya kimkakati.
“Nchi zenye utajiri wa madini haya hazina budi kukaa pamoja ili kutunga sera na sheria madhubuti za kusimamia madini haya, tumeona nchi zenye utajiri wa mafuta (Opec) zinafanya hivyo na usimamizi unakuwa mzuri,” anasema Oduk.
Oduk, ambaye taasisi anayoihudumu inajihusisha na tafiti na ufuatiliaji wa madeni na maendeleo barani Afrika, anasema utafiti walioufanya ulionyesha kuwa mahitaji ya madini ya kimkakati yanazidi kuongezeka kila siku na huenda hadi mwaka 2024 mahitaji yake yakawa ni mara mbili ya sasa.
Naye mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Abel Kinyondo anasema ili kuvuna manufaa iko haja ya kufanya mapitio ya kuangalia ni kwa namna gani sera na sheria zinatekelezwa ili kuhakikisha madini ya kimkakati yanakuwa na manufaa zaidi kwa Watanzania.
“Tunatunga sheria na tunakuwa na sera lakini je, tumewahi kukaa chini kujadili hizo sheria na sera zilizopo tunatekeleza kwa kiwango gani kuangalia madhara ya mikataba ya nyuma katika uwekezaji ili kuhakikisha rasilimali hizi zinanufaisha Watanzania,” anasema.
Mwelekeo muhamo wa nishati
Katika hotuba zake za hivi karibuni, Naibu Waziri Mkuu Doto Biteko, ambaye amewahi kuhudumu kama Waziri wa Madini alisema kutokana na mwelekeo wa dunia wa kutumia nishati safi, Tanzania itatumia rasilimali zake kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi ambazo ni matokeo ya matumizi ya nishati chafu.
Miongoni mwa rasilimali hizo ni gesi asilia na Dk Biteko alieleza kuwa mpaka sasa ugunduzi wa gesi nchini Tanzania ni futi za ujazo trilioni 57.54 na kati ya hizo, trilioni 47.4 zimegunduliwa eneo la kina kirefu cha bahari na trilioni 10.12 ambazo zimegunduliwa eneo la nchi kavu.
“Ugunduzi wa gesi ni fursa kubwa kwetu wakati tupo kwenye kampeni hii ya mabadiliko ya nishati kwenda kwenye matumizi ya nishati safi, kwani miongoni mwa changamoto kubwa zinazoisumbua dunia hivi sasa ni pamoja na mabadiliko ya tabianchi,” alisema Dk Biteko.
Hata hivyo, Dk Biteko alisema katika mabadiliko hayo ni muhimu sana kuangalia uhalisia wa kiuchumi wa watu, kwani kwa kiasi kikubwa matumizi ya nishati safi yana gharama kubwa kuliko nishati itumikayo hivi sasa.
“Nishati safi tunaihitaji sana, lakini tutaendelea kutumia nishati nyinginezo kuleta maendeleo, hususan upatikanaji wa umeme. Tutaendelea na vyanzo vya sasa kwa sababu tunahitaji kubadili hali za watu wetu,” alisema Dk Biteko.
Nishati safi uhalisia wa kiuchumi
Mshauri wa Masuala ya Uwekezaji na Biashara za Kimataifa, Reselian Manaiya Manaiya anasema matumizi ya nishati ya jadi (kisukuku) yanatoa faida za haraka kwa uchumi, yakichochea ukuaji wa haraka, kuunda ajira, na kuimarisha sekta za ndani. Anashauri Tanzania kutumia fursa hii.
“Hii inatoa msingi mzuri wa mustakabali endelevu kwa kuwekeza katika vyanzo vya nishati jadidifu,” anasema.
Aidha, hata katika uchimbaji wa Tanzania bado inaweka nguvu katika uchimbaji wa madini ambayo yanatajwa kuwa siyo rafiki wa mazingira.
Wakati wa hotuba ya bajeti ya mwaka 2024/25, Waziri wa Madini, Antony Mavunde alisema kuwa jumla ya vibali 11,258 vya kuuza madini nje ya nchi vilitolewa mwaka 2023 ikilinganishwa na vibali 10,318 mwaka 2022.
“Ongezeko la vibali hivyo kwa kiasi kikubwa limetokana na kuongezeka kwa uhitaji wa madini ya vito na makaa ya mawe nje ya nchi,” alisema Mavunde.
Aidha, Mavunde alieleza kuwa Shirika la Madini (STAMIKO) litaendelea na uzalishaji mkubwa wa makaa ya mawe katika eneo la Kabulo-Kiwira, ambapo tani 600,000 zimepangwa kuchimbwa mwaka 2024/25.
Kwa kuimarisha uzalishaji, Shirika limepanga kununua vifaa vipya, ikiwemo dump trucks, buldozer na excavators. Pia, Mavunde alibainisha kuwa kampuni ya Adan Group kutoka India itazalisha umeme wa megawati 2,000 kwa kutumia makaa hayo, ambapo upembuzi yakinifu utafuatilia gharama za uwekezaji na mashapo yanayopatikana.