Samia asimulia jinsi alivyompa Mafuru ‘urais’

Dar es Salaam. Alikuwa zaidi ya mtendaji wa kawaida serikalini, hivi ndivyo Rais Samia Suluhu Hassan alivyomzungumzia Lawrence Mafuru akimwona kama mtu ambaye mara kadhaa amelinasua Taifa katika hali ngumu.

Rais Samia amemwelezea Mafuru (52), aliyekuwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango alipowaongoza waombolezaji kuaga mwili wake, leo Alhamisi, Novemba 14, 2024 katika Uwanja wa Karimjee, jijini Dar es Salaam.

Mtaalamu huyo wa uchumi aliyefanya kazi sekta binafsi na umma alifikwa mauti Novemba 9, 2024, Hospitali ya Apollo, nchini India alipokuwa akipatiwa matibabu ya saratani ya damu. Mwili wake, utazikwa kesho Ijumaa makaburi ya Kondo yaliyopo Tegeta, Dar es Salaam.

Rais Samia amesema alipopata taarifa ya kifo chake alikumbuka mambo mawili makubwa ambayo mtendaji huyo aliyafanya kwa mustakabali wa Taifa ndani ya sekta binafsi na umma.

Samia amesema Machi 19, 2021 alipoingia madarakani baada ya kifo cha mtangulizi wake, John Magufuli, Mafuru alikuwa miongoni mwa washauri wake wa masuala ya uchumi.

Amesema Mafuru alikuwa miongoni wa wajumbe wa kamati wa kushughulikia changamoto ya Dola na aliifanya kazi hiyo kwa ufanisi mkubwa kwa kushirikiana na wenzake.

“Tulipopata changamoto ya Dola niliunda kamati ya kushughulikia suala hilo, kamati iliongozwa na Msajili wa Hazina Nehemia Mchechu akisaidiwa na wengine akiwemo Mafuru.

“Nakumbuka siku ya kutoa wasilisho lao mbele yangu, Mafuru aliniambia tukiufuata mpango huu kama tulivyouleta nchi itaondokana kabisa na tatizo hili na leo kila mmoja anaona, badala ya kuzibembeleza benki kutupa Dola sasa benki zinatuita tukachukue Dola kwao,” amesema Rais Samia.

Amesema kwa sasa amesikia wazalishaji malalamiko kwamba nchi haina Shilingi,”Sasa mpango wa kurudisha shilingi ndugu yetu ameondoa, nitawatumia waliokuwepo.”

Jambo lingine ambalo bado lipo kichwani mwa Rais Samia ni namna Mafuru alivyomshauri wakati nchi ilipokumbwa na changamoto ya miradi kwenye sekta ya ujenzi.

“Niliitisha kikao pale Zanzibar na kujadili mambo mengi baada ya kujadiliana nikawauliza hivi katika hali hii tuliyofika, kati yenu mmoja angekuwa Rais mungeamuaje na nikasema leo najivua urais sasa hivi nampa Lawrence Mafuru.

“Nikamwambia Mafuru nyanyuka wewe sasa ndio Rais, kwenye hali kama hii ungefanyaje. Alisimama kwa unyenyekevu mkubwa akaniambia mheshimiwa mimi si Rais na urais uko mbali nami,” amesema na kuongeza.

“Lakini katika hali kama hii akatoa mchango wake ambao hakika ulitutoa pale tulipo na tukaweza kusonga mbele,” amesema Rais Samia huku makofi yakipigwa ikiwemo na wanafamilia huku akiongeza, anawaona maofisa wake wanafuta machozi wakikumbuka Mafuru alivyosimama na kutoa mchango wake na kututoa tulipokuwa.

“Hakika ndugu zangu nimepoteza, tumepoteza kwenye Taifa hili,” amesema akisisitiza, “Nitakuwa sijakosea nikisema Lawrence Mafuru ni mmoja wa mashujaa wa Taifa letu. Alikuwa na mchango mkubwa kwa sekta binafasi na ya umma na kote huko alikopita ameacha alama chanya isiyofutika.

Kuhusu jukumu lake la uandaaji wa Dira ya Taifa, Rais Samia amesema Mafuru ameifanya kazi hiyo kwa ukamilifu mkubwa na siku si nyingi itawasilishwa kwa wadau kwa ajili ya kutoa maoni kabla ya kuanza kutumika.

“Niliyoyapokea kwenye dira ile yote ni mema kwa Taifa letu. Alikuwa mshauri mwema mwenye uwezo na hekima ya kushauri hata katika jambo ambalo hakubaliani nalo. Alikuwa na uwezo mkubwa wa kuwasiliana na umahiri mkubwa wa kuwasilisha hoja zake kwa staha, nidhamu na ushawishi,” amesema.

Mbali na hilo, Rais Samia amemtaja Mafuru kama mfano wa mtu uwezo wa kunyumbulika ili kuendana na muktadha.

Amesema Mafuru alithibitisha kwamba wadau wa sekta binafsi wanaweza kuwa na mchango mkubwa kwa umma wa Watanzania.

“Mafuru alianza kazi sekta binafsi kwenye sekta ya benki, ulipofanyika uamuzi wa kumleta kwenye sekta ya umma alionesha uwezo mkubwa wa kunyumbulika na kuweza kujifunza kwa haraka taratibu za Serikali bila kuathiri utendaji wake wa kazi aliotoka nao sekta binafsi,” amesema.

Rais Samia amesema miongoni mwa masomo ambayo Mafuru ameyaacha ni kila mmoja kutoa mchango wake wa hali na mali kadri Mungu alivyotujalia.

Related Posts