Dar es Salaam. Wafanyabiashara watatu akiwemo raia wa Malawi, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na mashtaka mawili ambayo ni kuongoza genge la uhalifu na kujaribu kuingilia mfumo wa kompyuta wa Benki ya CRDB.
Washtakiwa hao ni Joseph Wasonga (53) mkazi wa Mikocheni B, Franco Ruhinda (41) mkazi wa Tabata, na raia wa Malawi, Happy Shora (54) maarufu kama Show Show.
Wakili wa Serikali, Eric Davies amedai mahakamani hapo leo Alhamisi Novemba 14, 2024 kuwa washtakiwa hao wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 32350/2024 mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Godfrey Mhini.
Hata hivyo, kabla ya kusomewa mashtaka yao, Hakimu Mhini aliwaeleza washtakiwa hao mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza shauri hilo hivyo washtakiwa hawatatakiwa kujibu chochote baada ya kusomewa mashtaka yao.
Baada ya maelezo hayo, wakili Davies aliwasomea mashtaka washtakiwa hao.
Amedai kuwa katika shtaka la kwanza, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kuongoza genge la uhalifu.
Wanadaiwa tarehe na siku isiyofahamika ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, washtakiwa kwa makusudi waliongoza genge la uhalifu kwa kuingilia mfumo wa kompyuta wa benki ya CRDB kwa nia ya kuiba fedha.
Shtaka la pili ni jaribio la kutenda kosa linalowakabili washtakiwa wote.
Davies amedai washtakiwa hao wanadaiwa Oktoba 30, 2024 mkoani Mwanza, walifanya jaribio la kutenda kosa la kuingilia mfumo wa kompyuta katika benki ya ya CRDB.
Baada ya kuwasomewa mashtaka hayo, upande wa mashtaka ulidai upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika na kwamba wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutaja.
Hakimu Mhini ametoa masharti sita kwa ajili ya wadhamini. Moja, ametaka kila mshtakiwa awe na wadhamini wawili watakao saini bondi ya Sh5 milioni kila mmoja.
Pia, wadhamini hao wanatakiwa wawe na kitambulisho cha Taifa (Nida) pamoja na barua ya utambulisha kutoka taasisi wanayofanyia kazi au barua kutoka serikali za mitaa.
Masharti mengine, washtakiwa hao wanatakiwa kukabidhi hati zao za kusafiria mahakamani hapo.
Vile vile wadhamini hao wanatakiwa watoke Mkoa wa Dar es Salaam na sio vinginevyo.
Hakimu Mhini amesema pia, washtakiwa hao hawataruhusiwa kutoka nje ya mkoa wa Dar es Salaam.
Baada ya kutolewa masharti hayo, washtwakiwa wamedai hati zao za kusafiria zipo Polisi.
Kutokana na maelezo hayo, upande wa mashtaka ulipinga mahakama kutoa dhamana mpaka watakapojiridhisha iwapo, kama ni kweli hati za kusafiria za washtakiwa zipo Polisi Kitengo cha Uhalifu wa Kifedha (Financial Crime Unity-FCU).
Wakili Devies amepinga pia wasipewe dhamana kutokana na baadhi ya wadhamini kutoka nje ya mkoa wa Dar es Salaam huku wengine wakiwa hawana barua za utambulisho na kitambulisho cha taifa (Nida).
Hakimu Mhini amesema baada ya kusikiliza maelezo hayo, alikubaliana na pingamizi la upande wa mashtaka.
“Kutokana na maombi haya, Mahakama inahitaji kupata udhibitisho wa hati zao za kusafiria za washtakiwa hawa kutoka mamlaka husika,” amesema Hakimu Mhini.
Baada ya kueleza hayo, ameahirisha kesi hiyo hadi Novemba 26, 2024 kwa ajili kutajwa na washtakiwa wamerudishwa rumande.