SMZ yaondoa zuio uchimbaji mawe Pemba

Pemba. Kutokana na kilio cha wananchi kisiwani Pemba cha kuzuiwa kuchimba mawe, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imeondoa zuio hilo lakini ikiwataka kuzingatia utaratibu uliowekwa katika uchimbaji.

Kwa takriban mwezi mmoja SMZ ilizuia uchimbaji wa mawe ikiwa ni mkakati wa kukabiliana na uharibifu wa mazingira. Uamuzi huo ulilalamikiwa na wananchi wakieleza kukosa kipato.

Wakizungumza leo Novemba 14, 2024 Gombani, kisiwani Pemba ulikotangazwa uamuzi wa kuondoa zuio hilo, baadhi ya wananchi wamesema wamepitia wakati mgumu kuendesha maisha kutokana na zuio hilo.

Abdalla Mohammed Faki, amesema zuio hilo limemuathiri kwa kuwa hana kazi nyingine ya kufanya.

Ameiomba Serikali kuweka utaratibu maalumu wa uchimbaji mawe na siyo kuweka zuio kwa kuwa kazi hiyo ndiyo inayowapatia kipato cha kuendesha familia.

Kwa upande wake, Hamad Mkubwa amesema licha ya uwepo wa uharibifu wa mazingira, Serikali iweke mkakati maalumu wa upandaji miti kwenye maeneo yaliyotumika kuchimba mchanga na mawe.

Waziri wa Maji, Nishati na Madini, Shaibu Hassan Kaduara amesema Serikali imewaruhusu kuendelea na shughuli zao, kikubwa inawasisitiza kutunza mazingira kutokana mabadiliko ya tabiachi.

Amesema Serikali inatambua kuwa kazi hizo ni sehemu zao za kujipatia kipato lakini ni vyema kuzingatia athari za kimazingira.

Waziri amewataka kufukia mashimo ili ardhi itumike kwa shughuli zingine.

“Tumeamua kuondoa zuio la uchimbaji wa mawe ili kuwapa fursa wananchi kuendeleza shughuli zao za kiuchimi lakini wanapaswa kuzingatia utunzaji mazingira kwa kupanda miti ili kudhibiti athari za kimazingira,” amesema.

Related Posts