Dar es Salaam. Wakati Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akitarajiwa kufungua mkutano wa sita wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini Tanzania mwaka 2024 jijini Dar es Salaam, mada nane zitajadiliwa kwenye mkutano huo.
Mkutano huo wa siku tatu utaanza Novemba 19, 2024 ukiwaleta pamoja washiriki 1,500 kutoka ndani na nje ya Tanzania.
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amesema miongoni mwa watakaoshiriki ni Mawaziri wa Madini kutoka nchi za Afrika, watendaji wakuu wa kampuni kubwa za madini duniani zilizowekeza na zinazotarajia kuwekeza Tanzania.
Miongoni mwa kampuni hizo ni, BarrickGold, AngloGold Ashanti, Life Zone Metals, ShantaGold, Eco Graph, Faru Graphite, HeliumOne, Lindi Jumbo na Sotta Mining.
“Pia utashirikisha watafiti, mabalozi 31 wanaoziwakilisha nchi zao Tanzania, mabalozi wanaoiwakilisha nchi yetu nje ya nchi akiwemo Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Umoja wa Mataifa, Balozi Hussein Kattanga,” amesema.
Mavunde amesema mashirika ya kimataifa, waongezaji thamani madini, wafanyabiashara, taasisi za fedha, vyuo vikuu na vya kati, taasisi za umma na binafsi zinazojihusisha na shughuli za madini, viongozi mbalimbali wa kitaifa kutoka wizara, taasisi, mikoa, halmashauri na idara za Serikali pia watashiriki.
“Mkutano huu utakuwa na mada nane zitakazojadiliwa kutoka kwa watoa mada wabobezi kwenye sekta ya madini wapatao 20 wa nje ya nchi na 35 wa hapa nchini,” amesema.
Amesema mada zitakazojadiliwa zitagusia maeneo mengi ikiwemo changamoto zinazokabili masuala ya uongezaji thamani madini, fursa za uwekezaji na mitaji kwenye sekta ya madini, mikakati ya uendelezaji madini mkakati kwa ajili ya kuongeza manufaa ya mnyororo wa thamani.
Mada nyingine ni matumizi ya teknolojia katika uchimbaji mdogo wa madini, ushiriki wa wanawake na vijana katika sekta ya madini; kuendelea kutangaza madini adimu ya Tanzanite na masuala mengine yakiwemo uchimbaji bora na uhifadhi wa mazingira.
Mavunde amesema mkutano huo utafunguliwa na Rais Samia Novemba 19, 2024 na utafungwa na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi Novemba 21, 2024.
Amesema mbali shughuli hiyo kuvutia uwekezaji, unalenga kuweka msingi thabiti wa ushirikiano baina ya wadau, kuimarisha uzalishaji wa madini na kuhakikisha rasilimali hizi zinawanufaisha Watanzania kiuchumi na kijamii.
Amesema mkutano huo utaongozwa na kaulimbiu isemayo:“Uongezaji thamani madini kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii.”
Waziri huyo amesema kwa mara ya kwanza mwaka huu, tutaachana na utamaduni wa kuonesha bidhaa za madini ya vito pekee na kutokana na kaulimbiu yetu, tutagusa pia aina nyingine za madini yakiwemo ya viwandani na ujenzi, lengo ni kuonesha fursa zilizopo na kutambua matumizi ya madini katika maisha ya kila siku ya kiuchumi na kijamii.