TPA yatembeza vipigo SHIMMUTA | Mwanaspoti

Timu za Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) zinazoshiriki michezo ya SHIMMUTA inayoendelea mjini Tanga, zimekuwa moto wa kuotea mbali baada ya kutembeza vipigo mfululizo kwa wapinzani wake wakati mashindano hayo yakiingia raundi ya tatu tangu kuanza kwake.

Vipigo kwa wapinzani vilianza kutolewa tangu raundi ya kwanza ya kuanza kwa michuano hiyo, hali iliyoonyesha hakika mabingwa hao watetezi wa jumla wamepania kutetea mataji yao.

Wa kwanza kukutana na vipigo hivyo ilikuwa timu ya Tume ya Madini na Tume ya Nguvu za Atomic, ambapo ilinyukwa mabao 3-0 kwa upande wa soka, huku upande wa netiboli ikiibuka na ushindi wa vikapu 33-27 dhidi ya timu ya Tume ya Nguvu za Atomic.

Katika mchezo huo wa ufunguzi uliopigwa kwenye Viwanja vya Saruji nje kidogo ya mji wa Tanga, ilishuhudiwa TPA ikifungua akaunti ya mabao katika dakika ya kwanza ya mchezo kwa bao la ‘acrobatic ‘ lililofungwa na Ramadhani Madebe.

Bao la pili na la tatu lilifungwa na Said Jambae aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Madebe ambaye alipata majeraha yaliyomlazimu kushindwa kuendelea na mchezo.

Katika kile kinachoonekana kudhamiria kwa mabingwa hao watetezi kutetea ubingwa wao, timu za TPA zimeendelea kufanya makubwa katika mashindano hayo yanayoendelea jijini Tanga baada ya timu zake kutofungwa hata mchezo mmoja hadi sasa.

Ukianzia kwenye soka, timu yake ilifungua pazia la michuano hiyo Novemba 10,2024 kwa kuiadhibu Tume ya Madini jumla ya mabao 3-0, kisha kulazimishwa sare tasa na timu ya BMH kabla ya kuizabua DIT mabao 2-0 na ikaichabanga Ngorongoro 1-0.

Kwa upande wa netiboli, TPA ambao ndio mabingwa watetezi mechi ya kwanza walishinda 33-27 dhidi ya TAEC na mchezo wa pili walikutana na Chuo cha Tengeru (TICD) na kupata ushindi wa 33-14, mchezo uliofuata waliwatembezea mkong’oto DUCE kwa matokeo ya 32-13.

Upande wa Volleyball wanaume, TPA imeichapa timu ya Chuo cha Ardhi (ARU) kwa set 2-0 katika mchezo uliochezwa Novemba 13,2024.

Upande wa Kamba wanawake, timu ya TPA Novemba 13,2024, ilipata ushindi baada ya wapinzani wao timu ya TEA kuingia mitini.

Mashindano ya SHIMMUTA yameanza rasmi mjini Tanga, ambapo TPA imeshirikisha timu za michezo yote.

Katika mashindano yaliyofanyika mwaka jana mjini Dodoma, TPA iliibuka washindi wa jumla.

Related Posts