Mbali na kuzungumzia makabidhiano ya amani ya madaraka, Trump na Biden ambao ni mahasimu wa muda mrefu wa kisiasa, walijadili pia mizozo inayoendelea duniani ikiwa ni pamoja na vita vya Ukraine na Mashariki ya Kati.
Marais hao wawili ambao ukijumuisha umri wao unafikia miaka 159 walisalimiana huku Biden akionekana kutazama chini, wakati Trump akisimama kwa kujiamini na kumtazama Biden machoni.
Biden amkaribisha Trump Ikulu ya White House
Hata hivyo rais Biden amempongeza Trump kwa ushindi wake, wakati alimpokaribisha katika ofisi ya rais na kusalimiana naye kwa kushikana mikono, akimuahidi mchakato mzuri wa kumkabidhi mamlaka. Ikumbukwe kuwa miaka minne iliyopita, baada ya kushindwa katika uchaguzi, Trump alikataa kushiriki katika utaratibu huo wa kukabidhiana madaraka.
Msemaji wa Ikulu ya White House Karine Jean-Pierre, aliwaeleza waandishi wa habari kwamba viongozi hao wawili wamejadili masuala muhimu kuhusu usalama wa kitaifa na sera za ndani zinazolikabili taifa la Marekani na ulimwengu kwa ujumla.
Sullivan asema Biden alimsisitizia Trump kwamba ni muhimu kuendeleza uungaji mkono wa Marekani kwa Ukraine
Naye mshauri wa usalama wa kitaifa Jake Sullivan amesema Biden alimsisitizia Trump kwamba ni muhimu kuendeleza uungaji mkono wa Marekani kwa Ukraine dhidi ya uvamizi wa Urusi.
Kulingana na Sullivan, Biden amesema uungaji mkono kwa Ukraine ni bora kwa usalama wa taifa wa Marekani kwa sababu uwepo wa bara la Ulaya lililo imara na thabiti kutazuia nchi hiyo kujiingiza katika vita.
US kuiongezea Ukraine misaada kabla ya Trump kuingia madarakani
Itakumbukwa kuwa Trump ambaye anaendelea kupanga safu yake ya uongozi, aliahidi kuvimaliza kwa haraka vita vya Urusi na Ukraine bila hata hivyo kueleza ni jinsi gani angelifanikisha hilo. Rais huyo mteule amelieleza pia gazeti la New York Post kwamba yeye na Biden walizungumzia sana kuhusu mzozo wa Mashariki ya Kati kwani alitaka kufahamu ni wapi walipofikia.
Viongozi hao wawili wamekutana wakati matokeo ya uchaguzi yakiwa yamekiwezesha chama cha Republican kudhibiti mabunge yote mawili ya Baraza la Wawakilishi na Seneti na hivyo kuashiria kuwa Trump hatokuwa na vikwazo kutekeleza sera na mipango yake.