Moshi. Mwanamume aliyefahamika kwa jina la Hassan Ali (40) ambaye inadaiwa alitengana na familia yake kwa zaidi ya miaka 10, amekutwa amefariki kwa kujinyonga katika eneo la uwanja wa mpira wa Mandela, Kata ya Bomambuzi, Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro.
Inaelezwa kuwa usiku wa jana Novemba 13, 2024, mwanaume huyo alifika nyumbani wanakoishi watoto wake na bibi yao na kuomba kuwaona watoto ambapo aliambiwa aondoke arudi kesho yake na lakini asubuhi leo alikutwa amejinyonga.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amethibitisha kutokea tukio hilo, usiku wa kuamkia leo Alhamisi ya Novemba 14, 2024.
Kamanda Maigwa amesema walipata taarifa za kuwepo kwa mwili wa mwanaume huyo anayedaiwa kujinyonga na walipofika waliukuta mwili huo chini baada ya tawi la mti analodaiwa kutumia kujinyonga kuvunjika.
Amesema wanaendelea na uchuguzi kuhusiana na tukio hilo na kuwaomba wananchi wenye taarifa zinazoweza kusaidia upatikanaji wa taarifa sahihi kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo.
“Tunachunguza chanzo cha tukio hili, tunaomba wananchi wenye taarifa zinazoweza kusaidia uchunguzi wa tukio hili watoe ushirikiano kwa jeshi la polisi, kwa sababu jirani kutoka hapa kuna ndugu zake, tunataka kuchunguza mienendo yake kuanzia jana na inasemekana ana mke, tutafuatilia na ndugu wengine,” amesema.
Ameongeza: “Lakini pia jirani hapa kuna nyumba ina kamera ya CCTV, tutachunguza kuona uwezo wake unaishia wapi ili kubaini kama inaweza kutoa mwanga juu ya kilichotokea,” amesema Maigwa.
Mtoto wa marehemu asimulia
Akizungumza tukio hilo, mmoja wa watoto wa marehemu, Ali Hassani amedai baba yao aliacha familia miaka 10 iliyopita na kuhamia kwa mke mwingine.
Amedai kuwa Novemba 13, 2024, usiku, alifika nyumbani walikokuwa wakiishi wadogo zake na bibi yao, akisema anataka kuwaona watoto ambapo bibi alimtaka aondoke arudi kesho yake (leo).
“Baba aliiacha familia miaka 10 iliyopita na kwenda kwa mwanamke mwingine ambaye naye nimembiwa wametengana hivi karibuni, lakini jana usiku (Novemba 13) alifika nyumbani akisema anataka kuwaona wadogo zangu, bibi akamwambia arudi kesho (leo) kwa sababu ilikuwa ni usiku mkubwa na walikuwa wamelala,” amesema Ali.
Ameongeza kuwa: “Baada ya kuambiwa hivyo na bibi, aliondoka lakini leo asubuhi tumepewa taarifa kuwa amekutwa amefariki kwa kujinyonga.”
Juma Msuya, mkazi wa eneo hilo, amesema alipokea taarifa saa 12:25 asubuhi kuhusu tukio hilo na alipofika hakuweza kumtambua marehemu, lakini baadhi ya watu wanadai ni fundi gereji eneo la Stendi ya Mboya, Manispaa ya Moshi.