Arusha. Hali ya sintofahamu imejitokeza katika uchaguzi wa viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Mkoa wa Arusha, baada ya baadhi ya wanachama wao kuleta vurugu wakituhumu uchaguzi huo kughubikwa na rushwa.
Aidha wamemtuhumu pia Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema, kuwa na wagombea aliokuwa anawapambania akitaka washinde katika uchaguzi huo.
Wakizungumza usiku wa kuamkia leo Alhamisi Novemba 14, 2024, baadhi ya wanachama hao wamedai kufukuzwa kufuatilia uchaguzi huo na kuwa hawatakubali kuchaguliwa viongozi wasiowataka.
Akizungumza nje ya ukumbi uliokofanyika uchaguzi huo, mmoja wa wanachama wa Chadema Jimbo la Arusha, Boniface Kimario, alidai kuwa uchaguzi huo umeghubikwa ya rushwa ya kutosha huku akidai Lema kupanga nani awe kiongozi.
“Mnamtetea Lema nini, wanatuharibia hiki chama hamasa ninyi mnapewa maelekezo ya kuzima taa miaka yote leo Lema hanijui mimi anaagiza mimi niumizwe, kumshambulia mtu ni kosa, hamasa aliyenishambulia ameagizwa na Lema,”amedai
“Mimi nimepigwa mateke nimeumizwa, hamasa aliyefanya hivyo ameagizwa na Lema huu uchaguzi umeanza asubuhi, umeahirishwa kuna press (mkutano na waandishi wa habari), baada ya press kwa sababu wana malengo yao wameagiza taa zizimwe kwa sababu wana malengo yao,”amedai.
Boniface amedai kuwa watu wameingizwa ukumbini na kutakiwa kupiga kura kwa maelekezo na kuwa wajumbe wametakiwa kupiga picha ya kura walizopiga katika uchaguzi huo jambo ambalo ni kinyume na utaratibu.
“Huu ni uchaguzi wa mkoa kila mtu ana haki ya kushiriki na kushuhuduia kiongozi wanayemtaka ni haki ya kila wmanachama,tumekuja wametuambia tuka nje wakaridhika,” amedai Boniface
“Huu ukumbi tuna kumbukumbu nao ulizimwa taa kwenye uchaguzi wangu ulizimwa taa mara tatu matokeo yakabadilika. Leo (jana ) tumeenda kununua taa kuzuia hili jambo lisitokee, kuja na taa hapa, Lema anaagiza hamasa wanitoe nje na nitawashitaki kwa majina yao,” alidai.
Boniface alidai kipindi cha nyuma chaguzi kama hizo kulikuwa kunawekwa mpaka televisheni na ambao siyo wajumbe kama wao wanaangalia kinachoendelea ndani ila uchaguzi wa mwaka huu wamezuiwa na kufukuzwa.
“Huu siyo uchaguzi wenye kuzingatia demokrasia, tumekubaliana na yote hayo, tunataka tuzuie taa isije ikazimwa bado Lema anaagiza tuumizwe na tupigwe, hiki chama kila mtu amedondosha jasho lake, kila mtu ametoa mchango wake kwenye hiki chama, wasiseme kuna kundi la wahuni, wote wanaogombea wana sifa sawa,”amedai.
“Huu uchaguzi umeghubikwa na rushwa ya kutosha, Lema amekuwa akipanga nani awe kiongozi lakini chama chenye katiba viongozi wanatokana na katiba siyo mtu,hatuwezi kusema CCM itoke madarakani halafu sisi hatuonyeshi mfano, uchaguzi unatakiwa kuwa huru na wa haki,”ameongeza.
Akizungumza kwa njia ya simu na Mwananchi leo Alhamisi Novemba 14, 2024, Lema amesema atazungumzia suala hilo kwenye uchaguzi wa viongozi Mkoa wa Manyara unaofanyika leo wilayani Babati.
“Unaweza ukatuma mwandishi wenu niko njiani ninakwenda Manyara kwenye uchaguzi nitatoa statement (taarifa) kwenye hotuba ya ufunguzi,” amesema.
Uchaguzi huo ulisimamiwa na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Bara, Benson Kigaila, aliyekuwa akisaidiwa na Katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa.
Akizungumzia tukio hilo, Golugwa amedai kuwa kuna watu wasiohusika ambao hawakuwa wajumbe hawawezi kuingia kwenye uchaguzi, kanuni zinataka wajumbe peke yao ndiyo wanaruhusiwa.
“Kuna watu kwa sababu ambazo hatukuwa tumezielewa waling’ang’ania kutaka kuingia kwenye uchaguzi, mfano uchaguzi wa wanawake wanaingia wanawake peke yao, kuna baadhi ya wanaume walitaka kuingia kwenye uchaguzi wa wanawake pia kuna watu ambao kwenye mchujo walikatwa, kwa sababu za kikanuni baadhi yao waliendelea kubeba hisia kwamba wanaonewa,”amedai.
“Kwa mfano Baraza la Vijana linahitaji vijana kuanzia miaka 30 na usizidi miaka 35 kwenye uongozi, sasa mtu hana hicho kigezo. Kilichofanyika ni kuwazuia wanachama wachache, kwenye vyama hivi kuna watu wa kila namna hata wehu na wendawazimu tunao,wengine walikuja wamelewa,” amesema.
“Walizuiwa na walipotaka kutumia nguvu, nguvu zilitumika kuzuia, kwa hiyo walizuiwa hatuwezi kusema tumepigana. Huu ndiyo ufafanuzi halisi, dunia nzima kanuni za uchaguzi zinataka wajumbe pekee ndiyo waingie kwenye kikao, ni wendawazimu mtu anang’ang’ania awepo,”ameongeza Golugwa.
Katibu huyo amedai kuwa baada ya wanachama hao kuondolewa, uchaguzi uliendelea vizuri na kumalizika kwa amani ambapo aliyechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Mkoa ni Elisa Mungure, Katibu Viola Lazaro na Joyce Mukya kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha).
“Uchaguzi umeenda vizuri kwa amani, tumesimamia kwa haki bila shida, kwa hiyo hao wachache waliotengeneza drama ni wasumbufu tu ambao kwenye vyama vyote huwa wapo,”amesema.
“Kuhusu wapigakura kutakiwa kupiga picha kura zao, wasifanye wanachama wote sisi wa Arusha na wasimamizi wa uchaguzi sisi ni wajinga hadi Lema akatuendesha, hapana. Hayo ni maneno ya kutunga hayo, watu wamepiga kura zao kwa siri hiyo Sh300,000 mtu anatoa ya nini,?” alihoji
“Tumechangishana pale hela ya chakula, ukumbi wote sasa hiyo Sh300,000 kwa kura moja huyo si mwendawazimu amerukwa na akili, uchaguzi tumesimamia kwa taratibu zote ikiwemo uhakiki wa wajumbe, kura zimepigwa za siri zikahesabiwa hadharani watu ndiyo wamechagua mtu wao,”amedai
Golugwa amesema chama hicho kinatarajia kufanya uchaguzi wake wa viongozi Mkoa wa Manyara na baada ya kumalizika kwa uchaguzi wa mkoa huo, utafanyika uchaguzi wa viongozi wa Kanda ya Kaskazini.