Wachungaji, wahubiri wapimwe afya ya akili kabla ya kutoa neno

Mwanza. Baadhi ya wasomi wa Biblia na viongozi wa dini wameshauri kitengenezwe chombo kitakachofuatilia mienendo ya wahubiri na wachungaji pamoja na kuwapima afya ya akili kabla ya kuruhusiwa kuhubiri.

Ushauri huo ni kufuatia ongezeko la makanisa nchini ambayo wachungaji na wahubiri wake wanadaiwa kuwapotosha waumini wao kwa kutumia maandiko ya Biblia na kuwaaminisha vitu kama maji, udongo na mafuta kuwapa utajiri na kuwaponya.

Ushauri huo umetolewa leo Alhamisi Novemba 14, 2024 kwenye kongamano la kiukemene kujadili imani moja na mafundisho sahihi kwa ustawi wa binadamu lililoandaliwa na Chuo cha Biblia cha Kilutheri Nyakato kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (Saut) vyote vya mkoani Mwanza.

Akitoa mada kwenye kongamano hilo, Mkuu wa Idara ya Falsafa na Maadili chuo cha Saut Mwanza, Padri Innocent Sanga amesema Biblia haina tena utamu wa kuhubiri na hata umisionari umepoteza ladha kwa sababu umeingiliwa na wanyang’anyi wanaotumia vifungu vyake kutapeli waumini wao.

“Tutengeneze chombo…Tunapaswa kuwapima wachungaji vichwa vyao, afya ya akili, kuna wengine ni wagonjwa, wanadanganya watu kumbe hapa kichwani pameshaharibika…miaka na miaka pameshaharibika.

“Watu wanajaa kanisani, kumbe yeye ni mgonjwa. Je, tunajaribu kupima wachungaji vichwa vyao? Ushauri nasaha lazima tuuweke karibu na makanisa yetu ili mapadri, wachungaji tuweze kupimwa vichwa vyetu…Unapoenda kuhubiri lazima upimwe kichwa kwamba una akili sawasawa,” amesema Dk Sanga.

Amesema Biblia sasa imekuwa sio chombo cha kuwapeleka watu mbinguni badala yake imekuwa chombo cha kuchumia matumbo ya watu ambao wakikosa ajira wanajifunza Biblia kidogo, wanafungua kanisa, wanafanya biashara na kupata utajiri akisema taasisi za kikanisa zimevamiwa.

“Dini imekuwa sasa tunachumia matumbo yetu na si kuokoa roho za watu…hiyo ni fedha ya aibu kutumia Biblia kupata fedha halafu tunalaani mafisadi serikalini, ni hatari kabisa kuwa fisadi kwa kutumia maandiko matakatifu, Biblia imekuwa inatakatifuza fedha chafu,” ameeleza.

Amesema mambo yanayosababisha wahubiri wanapotosha watu ni elimu na kushindwa kutafsiri maana halisi ya maandiko huku akitumia mfano wa Mathayo sura ya saba, aya ya saba mpaka nane unaosema “Ombeni nanyi mtapewa, tafuteni mtapata, bisheni hodi mtafunguliwa…” kutumiwa na baadhi ya wachungaji kuwalaghai waumini.

“Nimeona mchungaji mmoja kutokana na elimu ya Biblia, anawafundisha watu kugonga milango ya watu kila siku, anasema ukigonga mara tano hautokosa (wanachotaka kupata) sasa hizi ndio tafsiri za Biblia? Ni elimu wanakosa, ni hatari kabisa,” amesema.

Amesema maaskofu wa madhebu yote wakiungana na kuanzisha chombo na kupata baraka ya Serikali kwa kuwa ina meno na nguvu ya kubana makanisa yanayotoa mafundisho potofu.

 “Sasa hivi kumekuwa na utitiri wa madhehebu, imekuwa ni fujo, ghasia siyo tu kwa makanisa makubwa, madogo, imekuwa pia ghasia kwa Serikali. Serikali imejikuta imechukua kazi nyingine ya kutatua migogoro inayojaa kwenye vikanisa vidogo vidogo na pia raia wa Tanzania wanadhurumiwa, wanaibiwa na kudanganywa na hata wengine kufia imani kwa kudanganywa, wengine wanakuwa masikini kabisa wa kutupwa, na hata wengine wananyimwa haki ya elimu kwa sababu wachungaji wamesema elimu haina maana kwa kwenda mbinguni,” ameongeza Padri huyo.

Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Magharibi Bukoba, Dk Abednego Keshomshara amewataka waumini wajihadhari na manabii wa uongo kwa kuwa mahubiri yao yamewafanya watu waamini imani ambayo inawakataza kufanya kazi wakitegemea miujiza.

“Maandiko yanasema asiyefanya kazi na asile…wengine wanafanya upotoshaji wa kulazimisha waumini watoe fedha,” amesema.

Makamu Mkuu wa Chuo cha Saut Mwanza, Profesa Costa Mahalu amesema mafundisho ya kiimani ni nguzo muhimu ya kumfundisha mwanadamu kuhusu maisha ya kiroho, kijamii, kiuchumi na kimaadili akiongeza kuwa kupitia idara ya falsafa na maadili chuoni hapo wanatoa elimu ya kupambana na mafundisho hayo.

“Tumejidhatiti kutoa elimu ya fikra tunduizi kama nyenzo ya kupambana na mafundisho machafu, tunafahamu fikra tunduizi si tu ni njia ya kufundisha wanazuoni na wana taaluma bali pia ni njia ya kukuza muelekeo wa kiroho na kijamii unaozingatia ukweli unaojengeka katika mafundisho sahihi,” amesema Profesa Mahalu.

Mwanafunzi wa thiolojia katika Chuo cha Biblia Nyakato, Venitha Silveri akiishauri serikali kuweka sheria dhidi ya watu wanaoibuka na madhehebu yao kutapeli pamoja na kushirikiana na maaskofu kufuatilia wachungaji na wahubiri walipotoka na kama wana vigezo vya kuhubiri ili kudhibiti wimbi la wachungaji wapotoshaji.

Related Posts