WACHEZAJI wa Tabora United akiwemo Yacouba Songne na Heritier Makambo wamepewa ahadi mbili zenye jumla ya Sh250 milioni na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha.
Ahadi ya kwanza ni watakapoifunga Simba katika mchezo wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara utakaochezwa Desemba 28, mwaka huu Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mkoani Tabora, watapewa Sh50 milioni.
Baada ya hapo, wakimaliza ligi msimu huu nafasi tatu za juu, basi watapongezwa kwa Sh200 milioni na kufanya jumla kuwa ahadi ya Sh250 milioni.
Mbali na hayo, tayari kiongozi huyo ametimiza ahadi yake ya kuwakabidhi wachezaji wa timu ya Tabora United shilingi milioni 20 baada ya kuifunga Yanga mabao 3-1 kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa Novemba 7 mwaka huu kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
Hafla ya kukabidhi fedha hizo ikiwa ni motisha kwa wachezaji wa timu hiyo ilifanyika usiku wa Novemba 13 mwaka huu kwenye viwanja vya Hoteli ya Orion iliyopo Manispaa ya Tabora na kuhudhuriwa na wakuu wote wa wilaya za Mkoa wa Tabora.
Akizungumza wakati wa kukabidhi fedha hizo kwa wachezaji wa timu hiyo, kiongozi huyo amesema Tabora United italindwa kwa nguvu zote na wataisimamia kuhakikisha inamaliza ligi kuu msimu huu nafasi tatu za juu.
“Timu hii tunailinda kwa wivu mkubwa kwa kuwa imetupa heshima mkoani kwetu na sisi kama viongozi tutaendelea kuisimamia kuhakikisha itafanya vizuri na kwa kuanzia tumesema kila mchezo watakaoshinda nyumbani na ugenini wataendelea kupata Sh10 milioni mpaka ligi itakapomalizika,” alisema na kuongeza.
“Kama tulivyosema awali Tabora ikishinda mchezo wa marudiano dhidi ya Simba basi tutatoa motisha ya Sh50 milioni, malengo yetu ya kumaliza ligi kwenye nafasi tatu za juu yakitimia tutaleta zawadi ya Sh200 milioni kwa wachezaji kuwapongeza kwa kazi watakayokuwa wameifanya.”
Awali Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Deusdedith Katwale akizungumza kwenye hafla hiyo alisema yeyote atakayejaribu kuihujumu Tabora United na kubainika atachukuliwa hatua.
“Tumesikia mengi tumesherehekea sana baada ya kuifunga Yanga kwa hiyo tutashuka daraja kwa sababu tutahujumiwa kwenye michezo yetu, mimi niseme serikali itaweka mkono wake na atakayebainika kuihujumu timu hii atachukuliwa hatua kali kwani Tabora United kwa sasa ni nembo ya mkoa,” alisema.
Nahodha wa Tabora United, Kelvin Pemba alimshukuru mkuu wa mkoa huo kwa motisha aliyoiahidi na kuitekeleza huku akibainisha kwamba watajituma kupata mwendelezo wa matokeo mazuri.
“Tunamshukuru mkuu wetu wa mkoa kwa hii motisha na sisi kama wachezaji ahadi yetu ni moja tu kucheza kwa kujituma kupata matokeo mazuri kwenye michezo iliyobaki na ushindi dhidi ya Yanga hautatufanya tubweteke na badala yake tutakazana na hatutakubali kufungwa kirahisi,” alisema.