Unguja. Wakati kiwango cha dunia cha ulaji samaki kikiwa kilo 21 kwa mwaka kwa kila mtu, Zanzibar imekivuka na kufikia wastani wa kilo 22 kwa mtu kwa mwaka.
Hayo yamebainika leo Novemba 22, 2024 katika mkutano wa mtandao wa Afrika kuhusu masuala ya usalama wa samaki na matumizi ya teknolojia ya uvuvi unaofanyika kisiwani hapa kwa siku tatu.
Akizungumza katika mkutano huo Novemba 14, 2024 Waziri wa Uchumi wa Buluu Zanzibar, Shaabani Ali Othman amesema kwa sasa kisiwa hicho kimefikia tani 100,000 kwa samaki waliovuliwa mwaka huu kutoka tani 80,000 mwaka 2023.
“Idadi hiyo ni kubwa kutokana na kuongezeka kwa ulaji wa samaki kwa wananchi wake kufikia kilo 22 kwa kila mwananchi mmoja kwa mwaka idadi ambayo ni kubwa kulinganisha na ulaji wa samaki duniani wa kilo 21 kwa mwananchi mmoja,” amesema.
Amesema wananchi wa Zanzibar wamefikia vigezo vya dunia kwa ulaji samaki kutokana na kuvuliwa wengi nchini.
Waziri amesema ulaji huo utasaidia upatikanaji wa protini kwa wananchi na kujenga afya nzuri.
“Mkutano huu ni jambo la faraja kufanyika hapa Zanzibar kwa vile visiwa hivi vimezungukwa na bahari na kuna wavuvi wengi,” amesema.
Mratibu na mtaalamu wa uvuvi, Hashim Chande Muumin amesema Serikali imetoa miongozo ya uvuvi kwa kuwataka wavuvi kuvua samaki waliokomaa kisheria kuepuka kuvua wachanga.
Amesema mkutano huo kufanyika Tanzania itanufaika na tafiti ambazo pia zitasaidia kuondoa matatizo yaliyopo.
Pia wananchi watapata teknolojia rafiki ambayo itapunguza upotevu wa samaki kwa wavuvi.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti, Uvuvi na Maliasili za Bahari Zanzibar (Zafiri), Dk Zakalia Ali Khamis amesema usalama wa samaki Zanzibar ni mzuri kwa mujibu wa tafiti walizofanya.
Amesema wamewafundisha wavuvi njia bora na salama za kuendesha uvuvi.
“Kwa hiyo ni lazima tujali usalama wa samaki ili watu waendelee kuwa na chakula bora na kiwango kizidi kupanda, hivyo tunakuwa na uvuvi na mazingira endelevu kusiwe na kitu kinachoathiri kingine,” amesema.
Sheria ya Uvuvi namba saba ya mwaka 2010 imeeleza wazi kiwango cha samaki kinachotakiwa kuvuliwa, hivyo taasisi hiyo inasimamia viwango hivyo.