AKILI ZA KIJIWENI: Ateba anaanza kuwapa kazi ngumu Simba

TETESI ambazo hapa kijiweni tumezinasa kuhusu Leonel Ateba ni Simba ilitumia kiasi kikubwa cha fedha ili kumsajili akitokea kule Algeria katika timu ya USM Alger.

Tunaweza kuamini kuhusu hilo la Simba kutumia gharama kubwa kumnasa mshambuliaji huyo kwani imesajili baada ya kuvunja mkataba wake tena na timu ya Kaskazini mwa Afrika.

Huwa sio kazi rahisi kwa timu ya Kaskazini mwa Afrika kukubali mchezaji anayepata nafasi katika kikosi chake kuondoka kwa fedha kiduchu hivyo hata kwa Ateba ushahidi wa kimazingira unatuaminisha hivyo.

Jambo la pili ni haraka ambayo Simba ilikuwa nayo katika kumnasa mchezaji huyo kwani dirisha la usajili lilikuwa linakaribia ukingoni huku Kocha Fadlu Davids akiwa ameshawasisitiza wasajili mshambuliaji maana waliokuwepo bado hawatoshi kuipa uhakika wa mabao timu yake.

Mwamba baada ya kutua alianza vizuri kweli na naamini hata tajiri wa Lunyasi akawa anafurahia hela aliyotoa kwa ajili ya kukichukua kifaa hicho cha Cameroon inaenda kihalali na hajapigwa.

Hata hivyo, sasa nini kinamsibu jamaa yetu Ateba hivi sasa maana amekuwa na ukame wa kufumania nyavu katika siku za hivi karibuni hasa katika mechi za ligi kuu.

Tunajua kila mchezaji kuna nyakati huwa anapitia kipindi kigumu lakini kwa levo ya Ateba anapaswa kujitahidi angalau asiwe anafikisha mechi zaidi ya tano tena za ligi kuu bila kufunga bao kwa vile ile hadhi yake anaishusha kimtindo.

Asipofunga atawafanya mabeki wa timu pinzani kuanza kumzoea na ikishafikia hatua hiyo ndiyo mambo yatazidi kuwa magumu kwake kwa vile atapoteza hali ya kujiamini na kucheza kwa wasiwasi jambo ambalo litamuathiri zaidi.

Kana kwamba haitoshi, anapokuwa hafungi anawaweka mashabiki wa timu yake kwenye simanzi kwani watakosa la kumtetea maana utamaduni wa soka letu ni kusifia cha kwako na kuponda cha jirani.

Related Posts