Wakati Yanga ikitangaza kuachana na Miguel Gamondi na msaidizi wake Moussa Ndaw leo, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limempa adhabu ya kifungo cha mechi tatu na faini ya Sh 2 milioni kutokana na utovu wa nidhamu.
Taarifa iliyotolewa na mtendaji mkuu wa Yanga leo, imeeleza kuwa Gamondi amevunjiwa mkataba wake kama ilivyo kwa Ndaw.
Hata hivyo taarifa hiyo haikueleza sababu za kuachana na Gamondi lakini habari za uhakika ambazo Mwananchi Digital inazo ni kuwa sababu ni mwenendo usioridhisha wa timu hiyo msimu huu.
Inaonekana kutokuwa siku nzuri kwa Gamondi kwani kuwekwa kando kwake kumetangazwa katika siku ambayo kamati ya usimamizi na uendeshaji wa ligi imetangaza uamuzi wa kumfungia na kumtoza faini kocha huyo kutokana na utovu wa nidhamu.
“Kocha mkuu wa klabu ya Young Africans, Miguel Gamondi amefungiwa michezo mitatu (3) na kutozwa faini ya Sh. 2,000,000 (milioni mbili) kwa kosa la kumsukuma na kumuangusha chini kocha wa viungo wa klabu ya Singida Black Stars, Sliman Marloene, baada ya mabishano yaliyotokea wakati timu hizo zikienda mapumziko katika mchezo tajwa hapo juu kwenye uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
“Adhabu hii imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 45:2(2.1) ya kuhusu Udhibiti kwa Makocha Ligi Kuu,” imefafanua taarifa hiyo.
Kamati hiyo ya usimamizi na uendeshaji wa Ligi pia imeipiga rungu Singida Black Stars kwa kukiuka kanuni za Ligi.
“Klabu ya Singida Black Stars imetozwa faini ya Sh. 2,000,000 (milioni mbili) kwa kosa la kuingilia mazoezi ya klabu ya Young Africans siku moja kabla ya terehe ya mchezo tajwa hapo juu.
“Timu ya Singida iliingia kwenye uwanja wa New Amaan Complex katika muda wa kikanuni wa klabu ya Yanga kufanya mazoezi, jambo ambalo lilivuruga programu ya mazoezi hayo ya Yanga ambayo yalikuwa yakiendelea, kinyume na matakwa ya Kanuni ya 17:45 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.
“Klabu ya Singida Black Stars imepewa Onyo Kali kwa kosa la kuwakilishwa na maafisa wanne (4) tu kwenye kikao cha kitaalam cha maandalizi ya mchezo (MCM), badala ya watano (5) kama ilivyoainishwa kwenye Kanuni ya 17:2(2.2) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.
Adhabu hii imetolewa kwa kuzingatia kanuni ya 17:62 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo,” imefafanua taarifa hiyo.