WAKATI maswali yakiibuka juu ya hatma ya kifungo cha aliyekuwa kocha wa Yanga, Miguel Gamondi pamoja na faini aliyotozwa na Bodi ya Ligi Tanzania, ambapo chombo hicho kimetoa ufafanuzi kikisema Yanga ndiyo itakayowajibika kumlipia faini.
Gamondi amefungiwa mechi tatu na kutozwa faini Sh2 milioni kwa kosa la kumsukuma na kumuangusha chini kocha wa viungo wa Singida Black Stars, Sliman Marloene baada ya majibishano yaliyotokea wakati timu hizo zikienda mapumziko katika mchezo uliopigwa Zanzibar.
Maswali kuhusiana na adhabu hiyo yanatokana na Yanga kuamua kuachana na Gamondi leo, ambapo kocha huyo hana mkataba na klabu hiyo.
Katika mchezo huo wa Ligi Kuu Bara, Yanga ilishinda kwa bao 1-0.
Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia kanuni ya 45:2(2.1) ya ligi kuu kuhusu udhibiti kwa makocha.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Almasi Kasongo amesema adhabu ya kulipa fedha aliyopewa Gamondi na Bodi hiyo italipwa kama ilivyotakiwa na mhusika.
“Mhusika ndiye anayesimamia adhabu yake kwa sababu inamhusu yeye. Kuhusu namna ya kulipwa sisi tunatakiwa kuikata Yanga na wao ndio watamalizana kama wanamlipia au watamdai,” amesema.
“Kuhusu adhabu ya kufungiwa ni ya kikanuni, hivyo kuhama nayo itategemea kanuni ya nchi husika (atakakokwenda) kama inatambua wanaweza kumuambia aendelee nayo japo sina uhakika sana kwani hii ni adhabu ya Ligi Kuu Bara.”