BoT kuimarisha usimamizi wa mikopo ya mitandaoni kwa manufaa ya wananchi

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imedhamiria kuimarisha usimamizi wa sekta ya fedha ili kuhakikisha kuwa sekta hiyo inabaki thabiti, imara, na stahimilivu, hatua inayolenga kuwezesha ukuaji wa uchumi wa taifa.

Hayo yamesemwa Novemba 14, 2024, na Kaimu Meneja wa Huduma Ndogo za Fedha wa BoT, Dickson Gama, wakati akifungua semina kwa wahariri na waandishi wa habari kuhusu usimamizi wa mikopo ya mitandaoni.

Katika semina hiyo, BoT ilibainisha kwamba imekuwa ikihusika na usajili, udhibiti, na usimamizi wa taasisi za huduma ndogo za fedha kwa mujibu wa Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya Mwaka 2018.

Gama alisema kwamba lengo la semina hiyo ni kujenga uelewa bora kwa waandishi wa habari juu ya masuala yanayohusiana na mikopo ya mitandaoni na changamoto zake.

“Ni jukumu la BoT kusimamia huduma ndogo za fedha nchini, na kwa kutambua umuhimu wa vyombo vya habari kama kiunganishi kati ya Benki Kuu na jamii, tunatumaini elimu hii itasaidia kuboresha utoaji na upokeaji wa huduma za fedha kwa usalama zaidi,” alisema Gama.

Changamoto katika utoaji wa mikopo mitandaoni

Gama alifafanua kuwa mikopo ya mitandaoni imekuwa ikikua kwa kasi kutokana na urahisi wa upatikanaji wake, lakini ukuaji huu pia umekuja na changamoto mbalimbali. Changamoto hizo ni pamoja na riba na gharama kubwa za mikopo, ukosefu wa ulinzi wa taarifa za wakopaji, na masuala ya kimaadili katika utoaji wa huduma.

“Kutokana na changamoto hizo, BoT imekuwa mstari wa mbele kutoa elimu kwa watoa huduma na wananchi kwa lengo la kuhakikisha huduma hiyo inakuwa na manufaa kwa pande zote,” aliongeza Gama.

Aidha, BoT imewaagiza watoa huduma za mikopo kuzingatia sheria, kanuni, na miongozo ili kuhakikisha mikopo inatolewa kwa njia inayokidhi viwango vya kisheria.

Kwa ujumla, BoT imesisitiza dhamira yake ya kuhakikisha sekta ya fedha inakuwa na mchango wa moja kwa moja kwa ustawi wa uchumi wa taifa na usalama wa kifedha wa Watanzania kupitia usimamizi thabiti wa huduma za mikopo mitandaoni.

Related Posts