Championship pameanza kuchangamka | Mwanaspoti

UHONDO wa Ligi ya Championship unaendelea kushika kasi ambapo baada ya leo kupigwa michezo mitatu, kesho itapigwa mingine mitatu kwenye viwanja mbalimbali, ili kuzisaka pointi tatu muhimu za kusaka tiketi ya kucheza Ligi Kuu Bara msimu ujao.

Mchezo wa mapema saa 8:00 mchana utapigwa Uwanja wa Nangwanda Sijaona Mtwara ambapo Mbeya Kwanza iliyoichapa Geita Gold mabao 2-0, itacheza na Maafande wa Polisi Tanzania iliyotoka kujeruhiwa mechi iliyopita dhidi ya Bigman FC kwa bao 1-0.

Biashara United iliyofungwa na African Sports bao 1-0, mechi iliyopita ugenini, itaikaribisha Mtibwa Sugar iliyotoka kuifunga Stand United mabao 2-0, kwenye Uwanja wa Karume Mara sasa 10:00 jioni huku Cosmopolitan ikicheza dhidi ya TMA.

Cosmopolitan iliyopoteza michezo mitano hadi sasa kati ya minane iliyocheza itakuwa kwenye Uwanja wa Mabatini Pwani huku wapinzani wao TMA ikiwa na kumbukumbu nzuri baada ya mechi yake ya mwisho kushinda mabao 3-1, dhidi ya Green Warriors.

Ligi hiyo itaendelea kesho Jumapili kwa michezo miwili kupigwa ambapo Maafande wa Green Warriors itakuwa kwenye Uwanja wa Mabatini Pwani kucheza na Mbuni iliyoichapa Cosmopolitan mabao 3-0, huku Mbeya City ikicheza dhidi ya Transit Camp.

Kocha wa Transit Camp, All Ally alisema ugeni wake katika kikosi hicho umechangia timu hiyo kufanya vibaya hadi sasa kwenye michezo minane waliyocheza, huku akiweka wazi changamoto nyingine pia imekuwa ni kushindwa kutumia vyema nafasi.

“Michezo minane bila ya ushindi kwa kweli hata sisi kama benchi la ufundi inatuumiza lakini licha ya yote ila hatujakata tamaa na tunaendelea kupambana kuangalia tunaondokana na hali hii, naamini ni upepo mbaya tu tulioanza nao,” alisema.

Related Posts