Mbeya. Wakulima wa mpunga katika shamba la Kapunga wilayani Mbarali, mkoani Mbeya walioathiriwa na mafuriko, wamekabidhiwa hundi ya zaidi ya Sh100 milioni ikiwa ni fidia kutokana na hasara waliyopata.
Mei, mwaka huu wakulima 195 katika shamba hilo mazao yao yaliathiriwa na mafuriko, kati yao 30 hawakuambulia chochote.
Mafuriko hayo yaliwaathiri zaidi waliokuwa na mikopo katika taasisi za kifedha, kutokana na hasara waliyopata walishindwa kufanya marejesho.
Kutokana na athari hizo, kampuni ya bima ya Strategis kwa kushirikiana na Benki ya Selcom imewakabidhi hundi ya Sh110.7 milioni. Wakulima hao ni wanachama katika taasisi hizo.
Wakizungumza jana Novemba 14, 2024 wakati wa hafla ya kukabidhiwa hundi hiyo, baadhi ya wakulima wamesema wamerejesha furaha na kuondokana na presha ya kuuza mali zao ili kulipa mikopo.
Jacob Mseleus, amesema hawakutarajia kupokea fidia hiyo kutokana na kipindi kigumu walichopitia.
Amesema sasa wanapata nguvu ya kuanza msimu mpya wa kilimo.
Mseleus amesema mara kadhaa wamekuwa wakisikia taasisi nyingi za mikopo huwatelekeza wanachama lakini imekuwa tofauti kwa kampuni hizo ambazo zimewarejeshea matumaini mapya.
“Mashamba yetu yalijaa maji mazao yakasombwa hatukuvuna kitu, tunashukuru tumepokea fidia sisi wakulima wenye bima. Tunakwenda kujipanga kwa msimu mpya,” amesema.
Mkulima mwingine, Oliver Alphonce amesema alikuwa katika harakati za kuuza nyumba yake ili kulipa mkopo lakini kupitia fidia hiyo, anaweza kukamilisha malengo yake na kuweka mipango mipya ya msimu wa kilimo.
“Mimi mnufaika wa bima za Strategis na mkopo wa Selcom leo nina furaha kuona ninarudisha matumaini mapya katika kilimo, tangu kukumbwa na mafuriko nimekuwa kwenye presha hadi kuwaza kuuza nyumba. Sasa naanza mipango mingine ya maendeleo,” amesema.
Mkuu wa kitengo cha biashara katika Benki ya Selcom, Isaya Mwenisongole amesema fidia hiyo inawalenga waliothirika na mafuriko, lengo ni kuhakikisha wanaendelea na uzalishaji.
“Walikuwa na malengo yao lakini kwa bahati mbaya mafuriko yaliwapiga, hivyo tumeamua kuwafidia kwa kuwa ni wanachama wetu na huu ndiyo utaratibu wa taasisi hii kwa wanachama wake,” amesema.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Strategis Insurance, Jabir Kigoda amesema kupitia programu ya bima mtetezi kwa wanachama wao, wanasaidia wakulima walioathirika na mafuriko, ukame na wadudu.
“Tuna wakulima 1,834 nchini, hapa walioathirika zaidi katika shamba hili ni 30 ambao watanufaika na fidia hii, lakini tunaendelea kutoa mikopo yenye riba nafuu.
“Tungeweza kukabidhi fedha hizi hata ofisini kwetu lakini kutokana na thamani ya wanachama wetu tumeamua kuwafuata shambani tujionee uhalisia,” amesema.