Israel yalaumiwa kwa mauaji ya halaiki – DW – 15.11.2024

Kamati hiyo Maalum ya Umoja wa Mataifa imeashiria idadi kubwa ya raia waliojeruhiwa na hali inayotishia maisha ya watu ambayo imewekwa kwa makusudi kwa Wapalestina, tangu wakati wa shambulio baya la Hamas la Oktoba 7, mwaka jana nchini Israel.

Soma Pia: Israel yatakiwa kutekeleza hatua za kusitisha mapigano Gaza 

Kamati hiyo imesema kwa Israel kulizingira eneo hilo, kuzuia misaada, mashambulizi ya kuwalenga watu na mauaji ya raia, licha ya amri ya Umoja wa Mataifa na ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) kupinga mambo hayo ni sawa na kusababisha kwa makusudi vifo, njaa na majeraha mabaya miongoni mwa watu.

Mashambulizi ya Israel | Jabalia, kaskazini mwa Gaza
Wapalestina katika eneo la Jabalia, kaskazini mwa Gaza lililoshambuliwa na IsraelPicha: Omar AL-QATTAA/AFP

Israel kwa upande wake imesema madai ya Shirika la Human Rights Watch ni ya ‘uongo kabisa’, ikisisitiza kwamba juhudi zake zinalenga tu katika kuusambaratisha uwezo wa kigaidi wa kundi la Hamas na sio kwa watu wa Gaza lakini Israel bado haijajibu ripoti ya Umoja wa Mataifa inayosema vita vya Israel katika Ukanda wa Gaza ni ‘mauaji ya halaiki’.

Soma Pia: Israel yaendeleza mashambulizi Gaza na lebanon

Tathmini iliyoungwa mkono na Umoja wa Mataifa ya mwishoni mwa juma ilionya juu ya baa la njaa katika eneo la kaskazini mwa Gaza linalokabiliwa na mashambulizi makali ya Israeli tangu mapema mwezi Oktoba.

Msemaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi wa Palestina, Louise Waterridge, ameliambia shirika la Habari la AFP kwamba operesheni ya Israel, imewalazimisha takriban watu 100,000 kukimbia kutoka kaskazini mwa Gaza kwenda kwenye maeneo ya karibu ili kuyanusuru maisha yao.

Soma Pia: Mashirika ya kiutu yasema Israel imeshindwa kuruhusu upelekaji misaada Gaza

Human Rights Watch, katika ripoti yake, iliyotolewa jsiku ya Alhamisi, imesema kulazimishwa watu kuhama kutoka kwenye makazi yao ni hatua ya makusudi na ni sehemu ya sera ya serikali ya Israeli na hivyo hatua hiyo ni uhalifu dhidi ya ubinadamu.

Nadia Hardman, Mtafiti, katika Kitengo cha Haki za Wakimbizi na Wahamiaji, cha shirika la Human Rights Watch amesema matokeo ya ripoti ya kurasa 172 yalitokana na mahojiano na watu wa Gaza waliokimbia makazi yao, picha za satelaiti na taarifa za umma zilizokusanywa hadi mwezi Agosti 2024.

Human Rights Watch | Joe Stork
Joe Stork, mkurugenzi wa Human Rights Watch kanda ya Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini,Picha: AFIN HAMED/AFP/Getty Images

Amesema ni muhimu kuyapinga madai ya Israeli kwamba inatii sheria za vita na kwamba inatakiwa kufuata kikamilifu sheria za kimataifa za haki za kibinadamu.

Soma Pia: Mwanamfalme wa Saudia bin Salman aitisha usitishwaji wa mapigano Gaza, Lebanon

Jeshi la Israel katika taarifa yake kwa shirika la Habari la AFP limekosoa na kulilaumu shirika la kutetea haki za binadamu la HRW kwa kuichukia Israel na pia kwa kutoa taarifa zilizo na upotoshaji wa wazi.

Marekani, mshirika mkuu wa Israel imesema haikubaliani na matokeo ya utafiti wa kamati ya Umoja wa Mataifa.

Chanzo: AFP

 

Related Posts