Mabehewa 264 ya mizigo SGR kuwasili Desemba

Shirika la Reli Tanzania (TRC) linatarajia kupokea shehena ya mabehewa 264 kwa ajili ya mizigo katika Reli ya Kiwango cha Kimataifa (SGR) katikati ya Desemba 2024.

Taarifa hiyo imetolewa leo Ijumaa Novemba 15, 2024 na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano wa shirika hilo, Fredy Mwanjala.

“Shirika la Reli Tanzania TRC linautaarifu umma kuwa utengenezaji wa mabehewa 264 ya mizigo yatakayotumika katika reli ya kiwango cha kimataifa SGR umekamilika nchini China. Meli iliyobeba mabehewa hayo imeng’oa nanga China Novemba 12, 2024 na inatarajiwa kufika Tanzania katikati ya Desemba 2024,” imesema taarifa hiyo.

Mwanjala ameongeza kuwa “katika mzigo huo kuna mabehewa 200 ya kubeba makasha (makontena) na 64 ya kubeba mizigo isiyofungwa (loose cargo).

“Shehena hiyo ya mabehewa 264 ni sehemu ya jumla ya mabehewa 1,430 ambayo kwa mujibu wa mkataba yanatakiwa kutengenezwa na kampuni ya CRRC.”

Katika kipindi hiki ambacho mabehewa hayo hayajafika, mizigo yenye uzito uliopitiliza hairuhusiwi katika treni hizo, abiria wa daraja la biashara anapaswa kuwa na mzigo usiozidi kilo 30, huku daraja la uchumi usizidi kilo 20.

TRC ilianza huduma za SGR kati ya Dar es Salaam na Morogoro Juni 14, mwaka huu na Julai 25 ilianza safari za Dodoma.

Related Posts