Baada ya Yanga leo Ijumaa Novemba 15, 2024 kutoa taarifa ya kumtimua kocha wao Miguel Gamondi bila kutaja sababu, mashabiki wa timu hiyo wamegawanyika katika mitandao ya kijamii.
Taarifa ya kuachana na Gamondi pamoja na aliyekuwa msaidizi wake Moussa Ndew imetolewa leo baada ya tetesi kuzagaa wiki nzima na uongozi wa Yanga umesema upo kwenye mchakato wa kutafuta kocha mwingine.
Hata hivyo, hali hiyo imeonekana kuwagawa mashabiki wa timu hiyo ambao wamekuwa na maoni tofauti.
Kupitia ukurasa wa Instagram wa Mwananchi, mashabiki waliotoa maoni yao, wengine wameonyesha kushangazwa na taarifa hiyo kutokana na mazuri ambayo kocha huyo alikuwa ameyafanya, lakini baadhi wakiona ni sahihi kutimuliwa kwake.
@Small_Odds ameandikia: “Nomaaa… Shughuli imeishaaaa ila mpira una mambo mengi jamaniii. Mazuri yote ya Gamondi yaani kufungwa mechi mbili tu daaah nimekumbuka ya Robertinho wa Simba.”
Naye @ngweta_homeappliances’s ameandika “Ila haya yote kasababisha Tabora utd na Azam fc hawa gongowazi fc sio wavumilivu.”
Kwa upande wa @br_mawii yeye ameandika: “Lamba lamba moja na nyuki tatu, huku @fikia_ndoto_zako_ akiandika: “Kafanya mazuri yake tumkumbuke kwahayo.”
Kwa upande wake, @mwita285 ameema Gamondi hakustahili kufukuzwa bali uongozi ndio unahusika na kusuasua kwa timu hiyo.
“Waliopaswa kufukuzwa wapo wanadunda na wana enjoy the life (wanaburudika) waliopaswa kushikiliwa kwa ghalama zozote zile ndo wanafukuzwa kweli the world is cycle (dunia duara), ukishangaa ya Simba utayaona ya yanga.
“Uongozi wa Yanga tunajua nyinyi ndo mmemleta Gamondi na mmeamua kumuondoa basi sawa ila mmetukosea sana mbona sisi tuliona Gamondi ni kocha mzuri sana yaani hata kama kuna makosa kafanya hakuna alternatives (njia mbadala) zingine zingetumika zaidi ya hiyo kumtimua,”ameandika.