Namungo inajengwa kivingine | Mwanaspoti

KOCHA Msaidizi wa Namungo, Ngawina Ngawina amesema wiki mbili za mapumziko kupisha mechi za timu za taifa kufuzu Afcon 2025 zinawasaidia kujenga kikosi cha ushindani huku akiitaja Mashujaa.

Namungo ambayo kwa sasa inanolewa na Kocha Mkuu, Juma Mgunda, msimu huu imekuwa haina mwanzo mzuri baada ya kucheza mechi 10 za ligi na kupoteza saba, huku ikishinda michezo mitatu ikikamata nafasi ya 13 kwenye msimamo.

Akizungumza na Mwanaspoti, Ngawina alisema wiki mbili walizozipata zimesaidia kuendelea kukijenga kikosi cha ushindani na wanapambana kujenga utimamu kwa wachezaji wao kabla ya kuivaa Mashujaa FC Novemba 23 mwaka huu ugenini.

“Hatujawa bora zaidi lakini haimaanishi tuna kikosi kibovu, timu ipo vizuri, kuna makosa madogo madogo yameonekana na ndiyo tunapambana nayo kipindi hiki cha mapumziko kabla ya kurudi kwa ligi,” alisema na kuongeza.

“Mchezo wetu unaofuata baada ya mapumziko tunakutana na Mashujaa FC ugenini, ni timu ambayo siyo rahisi, ili uweze kutoa upinzani unatakiwa kuwa na timu yenye utimamu, tumebaini hilo ndilo tunafanyia kazi mapema.”

Ngawina alisema wachezaji wao pia hawafurahishwi na matokeo wanayoyapata jambo lililowalazimu kufanya kikao cha pamoja na kushauriana nini wafanye ili waweze kurudi wakiwa bora na kuipambania Namungo iweze kufikia malengo ya kuendelea kushiriki ligi msimu ujao.

“Umoja uliofanyika kuanzia wachezaji na benchi la ufundi matarajio yetu ni kuona tunarudi tukiwa bora na kutoa changamoto kwa wapinzani wetu, hatutaki kuwa timu kibonde, akili zote kwa Mashujaa ambao tunatambua ni bora lakini sisi pia tutakuwa bora zaidi yao,” alisema Ngawina

Related Posts